• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
BURUDANI: Angiey Fresh alenga kuufikia ubora wa hali ya juu

BURUDANI: Angiey Fresh alenga kuufikia ubora wa hali ya juu

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

AMEPANIA kuinua kipaji chake cha uimbaji kufikia kiwango cha kimataifa apate kuinua jina la Kenya.

Huyo si mwingine bali ni Lydia Angela Adhiambo almaarufu Angiey Fresh.

Anaamini kwa juhudi na malengo anayojiwekea, atafikia kiwango anachokusudia ili awe miongoni mwa wanamuziki wa Afrika Mashariki wanaofahamika kote barani Afrika.

Baada ya nyimbo zake za awali kuitikiwa vizuri, Angiey Fresh anasema ana mipango kabambe ya kwenda Tanzania na Uganda kufanya shoo ambazo ana imani ndizo zitakazoanza kumtambulisha zaidi.

“Nimewahi kufika nchi hizo lakini kwa matembezi na sasa nafanya mipango ya kwenda kwa ajili ya kuimba,” akasema.

Anigiey Fresh anasema kamwe hatakubali kubakia kuimba nyumbani Kenya pekee lakini ana nia ya kusambaza mbawa zake sehemu nyinginezo Afrika Mashariki na kwingineko Afrika kabla ya kwenda kuonyesha ubora wake huko ng’ambo.

Msanii Lydia Angela Adhiambo ‘Angiey Fresh’. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Anasema anakubaliana kuwa bahari ya muziki ni pana na kuna papa na nyangumi wanaopenda kutesa dagaa lakini kwake japo anakumbana na changamoto si haba, hakubali kuvunjika moyo.

Anazidi kufanya bidii kuhakikisha anafika anapohitaji.

Akiwa katika mji unaotambulika maarufu kuwa wa kihistoria hasa kwa kuwa unavutia watalii kutoka nchi mbalimbali za dunia, Angiey Fresh anaamini ipo siku atafanikiwa kupata udhamini wa kwenda ng’ambo kujifunza mengi juu ya muziki.

Siku hazijapita nyingi tangu mwanamuziki huyo atoe kibao cha ‘Fanya’ na yuko tayari kudondosha wimbo wake mwingine wa ‘Daddy’ wakati janga la virusi hatari vya corona litakuwa limemalizwa.

“Nimeupangia wimbo wangu wa ‘Daddy’ kuuzindua kwa kishindo baada ya janga la corona na ruhusa ya watu kuchanganyikana itakapotolewa. Nina mategemeo makubwa ya wimbo huo kuitikiwa vyema,” akasema Angiey Fresh.

Msanii huyo alipenda muziki tangu utotoni akitunga nyimbo na kuziimba nyumbani, akitumai kupata mwanya siku moja kuopnyesha kipaji chake.

“Mwanya huo niliufikia hapo mwaka 2015 ambapo nilitoa kibao changu cha kwanza cha ‘Umbea’ kilichoitikiwa vizuri,” akasema.

Baadhi ya nyimbo zake alizoimba ni pamoja na ‘Tulia’, ‘Vuruga unanikoroga’, ‘Pewa’ na ‘Songa’.

Kibao chake na mwanamuziki Richy Ree cha ‘Nipe’ ndicho kilichofanya vizuri.

Angie Fresh amewahi kushirikishwa katika nyimbo za kuelimisha jamii akisaini mkataba na shirika la KEMRI chini ya MADCA wimbo anaotarajia kuuimba wa ‘Mentali’ unaohusisha wagonjwa wa akili.

Kwake, ana hamu kubwa ya kuimba na kufanya kazi na Nyota Ndogo pamoja na Masauti.

“Nitafurahi sana kufanya kazi na wanamuziki hao kwani ninafuatiliza sana nyimbo zao,” akasema.

Msanii Lydia Angela Adhiambo ‘Angiey Fresh’. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Kwa wasanii chipukizi wanapopata fursa ya kufungulia jukwaa vigogo wa muziki, huwa ni wakati wao wa kutamba mbele ya mashabiki wanaohudhuria shoo hizo.

Angiey Fresh aliwahi kupata nafasi ya kuimba kabla ya kina Susumila na Otile Brown kujitokeza kuimba mjini Kilifi wakati uliopita.

“Nilifurahi kuwa jukwaa moja na waimbaji hao kwani nilipata kutambulika,” akasema.

Anapendelea sana mtindo wa Afro-fusion na kuchanganya midundo ya Kiafrika.

Anawashauri mashabiki wa muziki wake wakumbuke kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 na kila mara wawe wenye kuosha mikono, wavae maski wanapotoka nje ya nyumba zao. Pia anawaambia wasubiri kwa hamu vibao atakavyotoa mwaka huu 2020.

Amewataka wanamuziki wa Pwani wadumishe umoja na kusaidiana katika kuinua vipaji vyao vifikie vya wanamuziki wa kimataifa.

Anaamini Kenya na hasa mwambao wa Pwani una waimbaji wenye tajriba za kufikia kutambulika kimataifa.

“Nina imani kubwa kama tukishikana, kupendana na kusaidiana, sisi waimbaji wa Pwani tutafika mbali na hata tutatambulika sio kanda hii ya Afrika pekee bali kote duniani,” akasema Angiey Fresh.

You can share this post!

Kenya yatenga mamilioni kufanikisha vita dhidi ya pufya

Wanasoka wa klabu za La Liga kuanza mazoezi ya pamoja...

adminleo