COVID-19: Wagonjwa 25 wapya visa jumla nchini Kenya vikifika 912
Na CHARLES WASONGA
WATU 25 zaidi wamepatikana na ugonjwa wa Covid-19 nchini Kenya ndani ya saa 24 zilizopita na kufikisha 912 idadi jumla ya visa vya ugonjwa huo kufikia Jumatatu.
Katika kikao na wanahabari katika makao makuu ya Wizara ya Afya, Waziri Msaidizi Rashid Aman ametangaza kuwa hakuna aliyefariki kutokana na ugonjwa huo katika kipindi hicho.
Kwa hivyo, idadi ya waliofariki imesalia 50.
Lakini habari njema ni kwamba wagonjwa 22 zaidi wamepona na kuruhusiwa kwenda nyumbani na kufikisha 336, idadi jumla ya watu ambapo wamepata afueni kufikia Jumatatu, Mei 18, 2020.
“Wagonjwa hao 25 wamebainika baada ya sampuli 1,139 kufanyiwa uchunguzi katika kipindi cha saa 24 zilizopita,” amesema Dkt Aman.
Miongoni mwao, 23 ni Wakenya na wawili ni Wasomali.
Takwimu zinaonyesha 23 ni wanaume na wawili ni wanawake.
“Mgonjwa mdogo zaidi ana umri wa miaka 22 na mkubwa zaidi ana umri wa miaka 56,” Dkt Aman amesema.
Kwa misingi ya kaunti ambako wagonjwa wapya wanatoka, sita wanatoka Kajiado, Mombasa (5) Nairobi (3), Kiambu (3), Kwale (3), Taita Taveta (2), Garissa (2) na Meru (1).
“Kaunti za Meru, Taita Taveta na Garissa ndizo kaunti za hivi punde kuandikisha visa vya Covid-19 nchini Kenya. Kwa hivyo, jumla ya kaunti 23 kati ya 47 zimeathirika kufikia sasa (Jumatatu),” Dkt Aman akasema.
Katika kaunti ya Mombasa, wagonjwa wapya wanne wanatoka Likoni na mmoja anatoka Nyali.
Katika Kaunti ya Nairobi, mmoja atatoka Githurai 44, Kawangware (1), na wawili wanatoka Starehe.
Na katika Kaunti ya Kwale watu hao watatu waliopatikana na virusi vya corona ni madereva wa trela katika mji wa mpakani wa Lunga Lunga sawa na Taita Taveta ambapo watu hao ni madereva wa magari yayo hayo ya kubeba mizigo.
Na watu wawili waliopatikana na corona katika Kaunti ya Garissa wako katika kambi ya wakimbizi ya Daadab.
Dkt Aman pia ametangaza kuwa madereva 53 ambao walipatikana na Covid-19 katika maeneo mbalimbali ya mpaka wa Kenya na Tanzania na wakakatazwa kuingia nchini.
Miongoni mwao ni Watanzania 51 na raia wawili wa Burundi.