• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
UBOMOAJI: Matiang’i na wenzake wakaidi seneti

UBOMOAJI: Matiang’i na wenzake wakaidi seneti

Na CHARLES WASONGA

MAWAZIRI watatu na Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Huduma Nairobi (NMS) Mohammed Badi wamefeli kufika mbele ya maseneta Jumatatu kujibu maswali kuhusu ubomoaji uliotekelezwa maeneo ya Kariobangi North na Ruai.

Mawaziri Fred Matiang’i (Masuala ya Ndani), Sicily Kariuki (Maji) na Farida Karoney (Ardhi) wamekosa kufika mbele ya kamati ya seneti kuhusu ardhi waeleze ni kwa nini nyumba za maelfu ya wakazi wa maeneo hayo zilizobomolewa wakati huu mgumu wa janga la corona.

Kufuatia swali ambalo liliulizwa na Seneta wa Nairobi Johnston Sakaja wiki jana, mawaziri hao walitakiwa kueleza ni kwani haki za wakazi hao zilkiukwa pamoja na agizo la mahakama la kusitisha hatua hizo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ya seneti kuhusu ardhi Mwangi Githiomi amesema mawaziri hao waliomba mkutano huo uahirishwe ili wapata muda wa kukusanya maelezo zaidi kuhusu suala hili.

“Mawaziri waliniambia kuna habari muhimu wanasaka na baada ya kuzipata tunaweza kupanga mkutano mwingine juma lijalo,” akasema Seneta huyo wa Nyandarua.

Hata hivyo, Bw Githiomi amesema hakupokea maelezo yoyote kuhusu ni kwa nini Meja Jenerali (mstaafu) Badi hakuheshimu mwaliko wa mkutano wake katika Majengo ya Bunge, Nairobi.

Hatua

Seneta Sakaja pia ametaka mawaziri hao kuwasilisha kwa seneti hatua ambazo zimewekwa kuhakikisha haki za raia hazivunjwi nyakati za ubomoaji wa majengo yaliyoko katika ardhi ya umma.

“Vilevile, nataka serikali ieleze hatua ambazo zimechukuliwa dhidi ya maafisa wake wanaohusika katika upeanaji wa ardhi ya umma na zilitengewa upanuzi wa barabara kinyume. Na muhimu zaidi nataka serikali iwalipe ridhaa raia walioathirika na ubomoaji eneo la Kariobangi North na Ruai,” akasema.

Zaidi ya familia 7,000 ziliachwa bila makao katika ubomoaji uliotekelezwa majuma mawili yaliyopita katika kitongoji cha Kariobangi Sewerage, Kariobangi North. Ardhi hiyo inasemekana kuwa mali ya Kampuni ya Maji na Majitaka Nairobi (NCWSC).

You can share this post!

COVID-19: Wagonjwa 25 wapya visa jumla nchini Kenya...

Obiri kustaafu riadha akivunja rekodi ya dunia katika mbio...

adminleo