YASIKITISHA: Badala ya mwangaza nyaya za stima zasababisha maafa mtaa wa mabanda wa Bangladesh
Na WINNIE ATIENO
NYAYA za stima zinaning’inia vibaya katika nyumba za wakazi wa mtaa wa mabanda wa Bangladesh, Mombasa na watoto wanazichezea pasi kujua hatari wanayoikodolea macho.
Hata hivyo, wakazi hao kwenye mahojiano wanasema wametoa wito kwa kampuni ya kusambaza umeme ya Kenya Power kushughulikia swala hilo, lakini miezi miwili baadaye “hakuna ilichofanya.”
Maafa yalibisha hodi Jumamosi ambapo watoto wawili walifariki baada ya kushika nyaya hizo hatari za umeme na mara baada ya mkasa huo kampuni hiyo ilifika na kuzirekebisha.
Wakazi wanaendelea kughadhabishwa na mkasa huo ambao uliwaacha wengine wawili wakiwa hali mahututi na hivyo kulazwa katika hospitali kuu ya Pwani.
Aidha wakazi wamenyooshea kidole cha lawama kampuni hiyo kwa kuchelewa kurekebisha nyaya hizo wakisema watoto wao wangalikuwa hai zingalirekebishwa mapema.
Mzazi kwa jina Simon Kabale amesema alimpoteza mwanawe Fridah Khavai aliyekuwa na umri wa miaka 10 na mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi ya St Peter huko Bangladesh baada ya kupigwa shoki na nyaya hizo.
“Nilipigiwa simu kwamba kulikuwa na ajali iliyowahusisha watoto katika eneo langu, nikawahi katika hospitali ya mmiliki binafsi huko Mikindani ambako nilitafuta mwanangu, lakini nikapata alikuwa ashaaga dunia. Nimesononeshwa na kisa hicho,” akasema baba huyo wa watoto watatu.
Akiongea na Taifa Leo huko Bangladesh, Bw Kabale alisema mwanawe ni miongoni mwa watoto waliohusika kwenye ajali ya nyaya za stima walipokuwa wakicheza.
Rafikiye marehemu alinusurika alipokuwa akijaribu kumwokoa kutoka kwenye nyaya hizo.
Kulingana na babake manusura, Bw Newton Magandi mwanawe Nixon Charo alikuwa anajaribu kumsaidia Fridah ambaye alikuwa ameshikwa na nyaya hizo.
“Lakini hakuweza naye akashikwa na nyaya hizo lakini akanusurika na anaendelea kupokea matibabu katika hospitali kuu ya Pwani,” akasema Bw Magandi.
Bw Kabale anasema amepoteza mtoto mtiifu, shujaa na mwenye bidii.
“Ninataka haki itendeke; hatuwezi kuzika watoto wetu sababu ya utepetevu wa kampuni ya umeme. Tangu Disemba tumekuwa tukiwalilia waje kurekebisha nyaya hizi lakini kilio cha mnyonge hakikusikika,” aliongeza.
Bi Monica Achieng na Bw Michael Onyango ambao mwana wao Dolan Onyango alipatikana ameuawa kwenye ajali nyingine ya nyanya za umeme siku hiyo ya Jumamosi na kuzikwa kesho yake Jumapili anailaumu kampuni hiyo ya huduma za umeme.
Bw Onyango anasema mwana wao wa kwanza alijaribu kumwokoa nduguye lakini akashindwa.
“Alimpiga kwa kutumia mbao lakini alikuwa ameshafariki. Mtoto wangu alikuwa akicheza akashika socket na akarushwa na umeme,” akaeleza Bw Onyango.
Haya ni majanga ambayo wakazi wamekuwa wakikumbana nayo kila kuchao.
Lakini mkurugenzi wa kampuni ya Kenya Power tawi la Mombasa Bw Hicks Waswa anasema ajali hiyo ilitokea kufuatia mmomonyoko wa udongo (earth movements) uliosababishwa na mvua inayoendelea kunyesha.
“Sehemu ya mkasa ni bondeni ambapo ilitikishwa kufuatia mvua kubwa. Mlingoti wa nyaya za kusambaza umeme uliondoka sehemu yake na watoto walikjuwa wakichezea waya wakakumbana na mauti. Inasikitisha,” akasema Bw Waswa.
Amewasihi wakazi kuwa makini na wakome kushika nyaya hizo.
Wiki hiyo hiyo mtoto mchanga aliaga dunia huko Bombolulu baada ya ajali ya nyaya za stima (electrution).
Afisa mkuu wa Nyali Bw David Masaba alisema mtoto huyo aliaga dunia baada ya kufikishwa katika kituo cha afya eneo la Ziwa la Ngombe.