ONYANGO: Ruto hana jingine ila kuunda chama kipya
Na LEONARD ONYANGO
NI bayana sasa kwamba, Naibu wa Rais William Ruto amepoteza ushawishi ndani ya chama cha Jubilee alichonuia kutumia kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Hii ni baada ya hasimu wake mkuu wa kisiasa eneo la Bonde la Ufa, Seneta wa Baringo Gideon Moi kukaribishwa ndani ya Jubilee.
Kutimuliwa kwa Bw Kipchumba Murkomen na Bi Susan Kihika kutoka wadhifa wa Kiongozi wa Wengi na Kiranja wa Wengi katika Seneti mtawalia pia ni pigo kwa Dkt Ruto.
Japo naibu wa rais anaonekana kupuuzilia mbali mambo yanayoendelea ndani ya Jubilee, ukweli ni kwamba kwa sasa yumo kwenye njiapanda. Njia anayofaa kuipitia kwenda Ikulu 2022 inazidi kuwa finyu na imejaa miiba.
Baada ya kufanikiwa kuwatimua Bw Murkomen na Bi Kihika, Rais Uhuru Kenyatta ambaye ni kiongozi wa Jubilee, sasa anadhibiti Kamati Kuu ya Chama (NEC).
Kwa mujibu wa katiba ya Jubilee, kamati ya NEC ndio hutoa uamuzi wa mwisho kuhusu mwaniaji wa urais atakayepeperusha bendera ya chama hicho.
Hivyo, kuna hatari kwamba, Dkt Ruto akiendelea kuwa ndani ya Jubilee akingojea kuteuliwa kuwa mwaniaji wa urais wa Jubilee huenda ikasalia ndoto.
Je, agure chama cha Jubilee? Hili ndilo swali ambalo linaonekana kusalia kitendawili kigumu kwa Dkt Ruto kutegua.
Swali hilo ni kitendawili kigumu kutegua kwa sababu kila hatua ambayo Dkt Ruto atachukua ina athari zake.
Iwapo ataamua kusalia ndani ya Jubilee, huenda akanyimwa tiketi ya chama hicho kuwania urais 2022 hivyo kufanya utabiri wa Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Francis Atwoli kwamba, Naibu wa Rais hatakuwa kwenye debe katika uchaguzi mkuu ujao, kutimia.
Iwapo ataunda chama kingine, kuna hatari ya kupoteza kura katika eneo la Mlima Kenya ambalo linaunga mkono chama cha Jubilee.
Kuunda chama kipya pia kutachukuliwa kwamba ametema Jubilee na kamati ya NEC inaweza kumtimua chamani hivyo kulazimika kujiuzulu wadhifa wake wa Naibu wa Rais.
Akijiuzulu kutoka wadhifa wake, huenda umaarufu na ushawishi wake wa kisiasa ukafifia.
Dkt Ruto anaweza kutafuta chama kilicho na uungwaji mkono katika maeneo ya Mlima Kenya kama vile PNU kinachoongozwa na Waziri wa Kilimo Peter Munya au Narc Kenya chake Bi Martha Karua na akitumie kuwania urais 2022. Hii ni kwa lengo la kunasa kura za Mlima Kenya.
Lakini changamoto ya kujiunga na chama cha watu wengine ni kwamba, viongozi wake wanaweza kuhongwa na kumnyima tiketi ya kuwania urais 2022 na kumwacha bila chama.
Ikiwa Naibu wa Rais anataka kusalia Jubilee, anapasa kuharakisha hatua ya kuenda mahakamani katika juhudi za kuzuia muungano baina ya chama hicho na Kanu. Lakini kuna uwezekano wa kesi hiyo kujikokota kwa zaidi ya mwaka mmoja hadi katika Mahakama ya Juu hivyo kupoteza wakati.
Ili kujiondolea masaibu ya kuachwa bila chama 2020, Naibu wa Rais anafaa kuunda chama chake mapema wafuasi wake wakizoee.