Presha zaidi kwa Ruto
Na CHARLES WASONGA
NAIBU Rais William Ruto sasa ‘anaumwa na kichwa’ kuhusiana na uongozi wa Bunge la Seneti.
Siku chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuwashawishi maseneta wa Jubilee kuwaondoa uongozini Kipchumba Murkomen (Kiongozi wa Wengi) na Susan Kihika (Kiranja wa Wengi), sasa mwandani mwingine, Naibu Spika Kindiki Kithure, anaandamwa.
Prof Kithure alikuwa mmoja wa mawakili wa Dkt Ruto akisidiana na Katwa Kigen. Inaaminika kuwa amekuwa mmoja wa nguzo kuu za Naibu Rais katika seneti.
Jumanne, Kiranja wa Wengi, Bw Irungu Kang’ata, aliwasilisha ilani ya hoja ya kumfuta kazi Prof Kithure, ambaye ni Seneta wa Tharaka Nithi.
Prof Kindiki alikuwa miongoni mwa maseneta waliosusia mkutano wa maseneta wa chama cha Jubilee ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi Jumatatu wiki jana.
“Naomba kuwasilisha notisi ya hoja kuhusu kuondolewa kwa Seneta Kithure Kindiki kutoka Afisi ya Naibu Spika,” akasema Bw Kang’ata ambaye ni Seneta wa Murang’a.
Sasa ni wajibu wa Kamati ya Kuratibu Shughuli za Seneti (HBC) inayoongozwa na Spika, kuamua ni lini hoja hiyo itajadiliwa na kupigiwa kura.
Kwa mujibu wa kipengee cha 106 (2)(c), hoja ya kumfuta kazi Naibu Spika wa bunge la kitaifa au seneti sharti iungwe mkono na thuluthi mbili ya wajumbe wote.
Kwa hivyo, hoja hii sharti iungwe mkono na maseneta 45 kati ya idadi jumla ya maseneta 67.
Akihojiwa katika kituo kimoja cha televisheni cha humu nchini Jumapili usiku, Bw Kang’ata alidokeza kuwa Jubilee inataka kumwondoa Prof Kithure kutoka wadhifa huo, wenye hadhi, kwa kudharua mwaliko wa kiongozi wa chama.
“Japokuwa alipokea mwaliko wa mkutano, aliamua kuususia bila kutoa sababu yoyote,” akasema Bw Kang’ata.
Ni katika mkutano huo uliosemekana kuhudhuriwa na maseneta 20 wa Jubilee, ambapo maseneta Kipchumba Murkomen na Susan Kihika walivuliwa nyadhifa zao.
Duru zinasema huenda wadhifa wa huo wa Naibu Spika ukapewa Seneta wa Uasin Gishu, Profesa Margaret Kamar ambaye alihudhuria kikao hicho.
Kando na Prof Kithure, Seneta wa Mandera Mahmuud Mohammed na mwenzake wa Laikipia John Kinyua pia huenda wakaondolewa kutoka nyadhifa za kuongoza kamati za Fedha na Ugatuzi, mtawalia.
Mnamo Jumatatu Bw Kang’ata alikutana na maseneta wa Jubilee kwa lengo la kuwashawishi waunge mkono hoja hiyo, ili idadi ya kumwondoa Prof Kithure ipatikane.