• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Mbunge wa Nyali ataka nguvu za wanasiasa zielekezwe katika kukabili Covid-19

Mbunge wa Nyali ataka nguvu za wanasiasa zielekezwe katika kukabili Covid-19

Na MISHI GONGO

MBUNGE wa Nyali Mohamed Ali sasa anasema mihemko ya kisiasa inayoshuhudiwa nchini si mizuri wakati huu taifa na ulimwengu unakumbwa na janga la Covid-19.

Akizungumza katika hafla ya ugavi wa chakula Jumanne mbunge huyo alisema si sawa kwa Rais Uhuru Kenyatta na vigogo wengine wa kisiasa kuangazia na hata kuzungumzia siasa za mwaka 2022 wakati nchi iko pabaya kutokana na athari za janga la corona.

Bw Ali alidai kuwa kwa sasa serikali chini ya uongozi wake Rais Kenyatta “inaelekea pabaya kufuatia kiongozi huyo kufanya njama za faraghani za kupanga atakayerithi kiti cha urais mwaka 2022 huku wananchi wakiendelea kutaabika kutokana na athari za janga la corona.”

Alidai kuwa mipango inayoendeshwa na Rais Kenyatta kuunda miungano ya kisiasa wakati huu ni kinaya kikubwa na badala yake nguvu hizo zingeelekezwa katika kupambana na athari za mafuriko, ubomoaji wa makazi ya watu katika maeneo mbalimbali ya nchi, ukosefu wa ajira na kudorora kwa uchumi.

Wakati huo huo alisisistiza kuwa Naibu Rais William Ruto bado yuko imara licha ya ‘njama za usaliti’ dhidi yake.

Alidai kuwa kwa sasa Ruto anaangazia zaidi namna ya kusaidia wananchi wakati huu wa janga la corona na kamwe hatojibu njama za kisiasa zinazoendeshwa dhidi yake.

Aliongezea kuwa licha ya kulengwa kwa baadhi ya viongozi wanaomuunga mkono Naibu Rais katika bunge la seneti na lile la kitaifa, mamlaka ya mwisho yanasalia kwa mwananchi mpigakura.

You can share this post!

Serikali yatangaza Mei 25 sikukuu ya Eid al-Fitr

Ujerumani yaifaa Kenya vituo viwili vya maabara tamba...

adminleo