Habari Mseto

COVID-19: Mbunge aitaka serikali iwasaidie wakazi wa Kibokoni

May 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Nyali, Bw Mohamed Ali ameitaka serikali kuwasaidia wakazi wa Kibokoni wanaoendelea kutaabika baada ya serikali kuu kufunga kijiji hicho kutokana na idadi ya juu ya visa vya maambukizi ya virusi vya corona.

Kijiji hicho chenye zaidi ya wakazi 20,000 kinaongoza kwa idadi ya watu walioambukizwa maradhi ya Covid-19 na hata vifo vinavyotokana na virusi vya corona Kaunti ya Mombasa.

Aidha ameitaka serikali ya kitaifa na ya kaunti kuweka mikakati madhubuti ya kuwasaidia wagonjwa wa Covid-19 na wakazi waliotatizika eneo hilo kwa sababu ya shughuli za kawaida kuyumbishwa.

Pia amemtaka Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho kuwaelezea wakazi namna alivyotumia fedha za ufadhili kulisha wakazi wa Mombasa.

“Kipindi cha mwezi mmoja uliopita wahisani walijitolea kusaidia waathiriwa wa virusi vya corona ilhali wakazi hususan wale wa Old Town wanaendelea kuteseka. Wakazi hawana kazi, wanadaiwa kodi za nyumba na changamoto kadha wa kadha. Serikali ya kaunti ina uwezo wa kupatia kila nyumba Sh100,000 au Sh50,000,” akasema Bw Ali akihutubia wanahabari jana Ijumaa.

Mbunge wa Nyali Mohamed Ali kwenye kikao na wanahabari Ijumaa, Mei 22, 2020, akizungumzia swala la virusi vya corona. Bw Ali alisema wakazi wanateseka kufuatia ukosefu wa chakula huku akimpa changamoto Gavana wa Mombasa Hassan Joho kuweka uwazi jinsi anavyoshughulikia suala hilo. Picha/ Winnie Atieno

Alitaka serikali ya kaunti kusimamia kodi za nyumba za watu eneo la Mji wa Kale – Old Town – ambalo limefungwa kutokana na idadi kubwa ya watu walioathirika.

Alisikitika kwamba wakazi wengi wanakeketwa na makali ya njaa, kero ya majitaka, taka, na ukosefu wa maji.

“Serikali isitumie janga hili na binadamu kama chambo cha kupata pesa,” akasema mbunge huyo.

Akaongeza: “Watu wa Kibokoni na Eastleigh jijini Nairobi wamewekewa polisi kila mahali, lakini wengi hawana chakula na kuna wazee wagonjwa mle ndani wanaougua kisukari. Serikali sharti iwe na mikakati ya kuwafaa?”