Kitoweo cha samaki chajileta Garsen lakini hakuna ugali
Na CHARLES LWANGA
BAADHI ya waathiriwa wa mafuriko katika kijiji cha Hewani eneobunge la Garsen wamelalama wakisema hawana ugali wa kuliwa pamoja na samaki wa matope waitwao ‘mtonzi’ ambao wameletwa na maji ya mafuriko ya Mto Tana.
Kijiji hicho ni kimojawapo cha vijiji 15 ambavyo Shirika la Msalaba Mwekundu (KRCS) limekitaja kwamba kimeathirika zaidi na mafuriko baada ya mto kuvunja kingo zake na maji kuzingira kijiji hicho.
Mkazi Bi Fibi Jilo anayejulikana kama ‘Mama Bahati’ amesema kuwa wakazi wanahangaika kwa kukosa chakula baada ya mashamba yao ya mahindi kuharibiwa na mafuriko.
“Sisi ni wakulima wa mpunga, lakini siku hizi tumeachana nao na kuanza kupanda mahindi ambayo nayo yameharibiwa na maji,” akasema.
Akihotubia mkutano ulioandaliwa na mbunge wa Garsen, Bw Ali Wario pamoja na uongozi wa serikali ya kitaifa kupeana vyakula vya msaada, Bi Jilo alisema licha ya kuvua samaki aina ya mtonzi, wakazi wangali hawana chakula cha kutosha.
“Ingawa tuna mtonzi ambao wameletwa na mafuriko, hatuna sima, mpunga wala chakula kingine ambacho tunaweza kutemremshia nacho samaki hao,” akasema na kuongeza “sisi sasa tumebakia kuwa watu wa kula samaki kila siku.”
Kwa upande wake, Bw Wario alisema tayari amejadiliana na mkurugenzi mkuu wa Tarda Irrigation scheme ambaye ameahidi kugawia wakazi vyakula vya msaada ambavyo vitawakimu kimaisha.
“Vilevile, serikali kuu pamoja na shirika la KRCS ambalo limezuru waathiriwa wako mbioni kutafuta na kugawa vyakula vya msaada,” alisema na kuongeza serikali imetenga Sh250 milioni katika bajeti ya mwaka ujao kukarabati miundomsingi kuzuia athari hasi za mafuriko.
Alisema anaelewa kuwa watu hula chakula aina tofauti tofauti kulingana na mila na tamaduni na kwamba atahakikisha wakazi wote walioathiriwa na mafuriko wamepata vyakula vya msaada.
Takriban watu 11,000 katika eneobunge hilo wameathiriwa na mafuriko ambayo tayari yamemeza vijiji vya Danisa, Galili na Bandi, huku yakiendelea kufunika kituo cha polisi cha Gamba na ofisi ya chifu wa Galili.
Baadhi ya wavuvi katika kijiji cha Hewani waliambia Taifa Leo kuwa wamechoshwa kula mtonzi bila chakula kingine kwa sababu hawawezi kuvuka mto uliojaa mamba bila dau kwenda Sokoni Garsen kuuza samaki hao.
“Imebidi tuvue wa kula mtonzi nyumbani pamoja na familia zetu; hawa samaki wamo tele humu ndani na mara nyingi sisi hugawia majirani,” alisema Bw Joshua Jilo.
Isitoshe, katika soko la Garsen, Taifa Leo ilipata baadhi wakazi wakiuza samaki hao ambao wanasema huwa wengi wakati wa mafuriko kwa bei nafuu kuanzia Sh50 hadi Sh300 kulingana na ukubwa na uzito katika mizani.