Thika Cloth Mills yayumbishwa na athari za Covid-19
Na LAWRENCE ONGARO
HALI ngumu ya mambo kufuatia janga la Covid-19 imefanya kampuni ya Thika Cloth Mills Ltd (TCM) iamue kufunga shughuli zake japo kwa muda.
Hatua hii imeathiri shughuli za kilimo cha pamba, malighafi ambayo wakulima walikuwa wakinufaika kupitia kuiuzia kampuni hiyo ya TCM, Sasa wamepata pigo kubwa.
Baadhi ya wakulima hao wanatoka maeneo ya Kitui, Yatta, na Homa Bay.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bi Tejal Dothia, alisema hata ingawa wamebanwa na hali ya uchumi, walitoa hundi ya Sh1 milioni katika hazina ya Covid-19 kuendea wanaopitia hali ngumu nchini.
Alisema kampuni hiyo ilikuwa ikishona nguo za walinda usalama na barakoa.
“Tumelazimika kuwapeleka nyumbani wafanyakazi wapatao 700 kwa lengo la kuzuia maambukizi ya coronavirus. Tunaelewa ugumu wa mambo lakini bado tutawajali baadaye,” alisema Bi Dothia.
Alitoa maelezo kwamba wangali katika orodha yao na mambo yakiwa mazuri watarejeshwa kazini.
Alisema tayari amejadiliana na benki tofauti kuona ya kwamba wafanyakazi hao wanapewa mikopo michache ili waweze kujikimu kimaisha.
“Hatungetaka kuwapoteza wafanyakazi hao kwani bado tunamikakati mingi tuliyokuwa tumeweka ili kuendelea kuboresha biashara yetu,” alisema mkurugenzi huyo.
Alisema kabla ya wafanyakazi hao kuambiwa waende nyumbani, kampuni hiyo ilikuwa imeshona barakoa kiasi kikubwa zilizosambazwa maeneo mengi ya Kaunti ya Kiambu.
Mnamo Novemba 2019 kampuni ya Thika Cloth Mills iliweza kuzuru kaunti za Machakos, Kitui, Homa Bay, na Siaya ili kuwahamasisha wakulima kuzingatia upanzi wa pamba kwa wingi.
“Nililazimika kuzuru maeneo hayo kwa sababu kampuni yetu inategemea pamba kwa kiwango kikubwa kwa kushona vitambaa na nguo,” alisema Bi Dothia.
Alisema wamekuwa wakihamasisha Wakenya kuzingatia mavazi yaliyoshonewa humu nchini, kwa usemi au kauli kuwa ‘Nunua Kenya na Ujenge Kenya’.
Alisema licha ya viwanda zaidi ya 10 kufungwa mjini Thika miaka ya tisini (1990s), kiwanda chao kimekuwa mstari wa mbele kunawiri licha ya pandahuka tele.
Kinara wa wafanyabiashara Bw Richard Ngatia alisema watafanya juhudi kuona ya kwamba kampuni mbili; Thika Cloth Mills na ile ya Small Medium Enterprises zinapokea fedha za kuinua biashara zao.
“Tunaelewa Covid-19 imesababisha masaibu mengi kwa kampuni nyingi lakini hali ikirejea shwari muungano wa wafanyabiashara utafanya juhudi kuona zinarejelea hali zao za hapo awali,” alisema Bw Ngatia.