• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
Duale hatarini zaidi kwa ‘undumakuwili’ wake

Duale hatarini zaidi kwa ‘undumakuwili’ wake

NA CHARLES WASONGA

BAADA ya Rais Uhuru Kenyatta kufaulu kuwang’oa wandani wa Naibu wake William Ruto kutoka uongozi wa Seneti shoka lake sasa linaelekezwa katika Bunge la Kitaifa.

Na Kiongozi wa Wengi Aden Duale ni miongoni mwa wanaolengwa kwa kile kilichotajwa kama “undumakuwili na kukosa heshima.”

Rais Kenyatta ameitisha mkutano wa kundi la wabunge wa Jubilee kabla ya Bunge la Kitaifa kurejelea vikao vya Juni 2, kwa matayarisho ya kusomwa kwa bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2020/2021.

Naibu mwenyekiti wa Jubilee, Bw David Murathe alithibitisha uwepo wa mkutano huo aliosema utatumiwa “kusafisha bunge la kitaifa.”

“Lazima Uhuru awe na mazingira safi ya kufanya kazi katika Seneti na Bunge la Kitaifa. Usafi huo sasa unaelekezwa katika bunge la kitaifa ambapo mkutano umeitishwa wa kuwaondoa wale ambao ni wakaidi,” akasema wiki jana kwenye mahojiano katika kituo kimoja cha redio.

Hata hivyo, hakutaja majina ya wale ambao wataondolewa lakini akasisitiza kuwa “tutakuwa na uongozi mpya bungeni kabla ya vikao kurejelewa.”

Japo inasemekana kuwa Bw Duale angesazwa wandani wa Dkt Ruto wanaoshikilia nyadhifa za uongozi katika bunge la kitaifa wakitimuliwa inahofiwa kuwa “undumakuwili” wake utaathiri ajenda ya Rais Kenyatta anapoelekea kukamilisha muhula wake wa mwisho mamlakani.

Duru zinasema japo Mbunge huyo wa Garissa Mjini amekuwa na uhusiano mzuri na Rais na Naibu wake, inadaiwa kuwa aliwashawishi maseneta wanaoegemea mrengo wa Dkt Ruto kususia mkutano ulioongozwa na Rais katika Ikulu ya Nairobi majuma mawili yaliyopita.

“Tuna habari kwamba yeye ndiye aliwachochea maseneta waliokataa kuhudhuria mkutano uliotishwa na Rais. Hii inaonyesha kuwa amekosa heshima kwa chama na uongozi wake,” akasema mbunge mmoja ambaye aliomba tulibane jina lake.

Lakini Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli Jumamosi alisema Bw Duale sharti apokonywe wadhifa wake katika mabadiliko yatakayofanywa katika uongozi wa Jubilee katika bunge la kitaifa.

Huku akishabikia kung’olewa kwa Naibu Spika wa Seneti Kithure Kindiki alisema mabadiliko hayo hayatakuwa makamilifu bila kutimuliwa kwa mbunge huyo wa Garissa Mjini.

“Hakuna haja ya kumwondo Profesa Kindiki na kumwacha Bw Duale katika Bunge la Kitaifa. Nitatumia rasilimali zangu zote kuendesha kampeni za kumwondoa,” Bw Atwoli akasema.

Lakini akimjibu kiongozi huyo wa COTU, Duale alisema nafasi yake bunge inalindwa na Katiba na haogopi kutimuliwa.

“Atwoli anapasa kufahamu kuwa siogopi kuondolewa. Je, anajua kuwa niko na historia ya kupigania mabadiliko? Atwoli anafaa kujua kuwa hana usemi wowote kuhusiana na wadhifa wangu kama kiongozi wa wengi kwa sababu sio mwanachama wa Kundi la Wabunge wa Jubilee (PG),” Bw Duale akanukuliwa akisema.

Alishikilia kuwa hatima yake itaamuliwa katika mkutano wa PG ya Jubilee chini ya uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto.

“Atwoli anapaswa kufahamu kuwa Duale hawezi kutishwa na matamshi yake,” Duale akaongeza.

Wengine ambao wanalengwa kuondolewa kutoka nyadhifa zao ni Kiranja wa Wengi Benjamin Washiali, Naibu wake Cecily Mbarire, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti Kimani Ichung’wa miongoni mwa wengine.

Bw Ichungwa alisema hana hofu ya kung’olewa mradi atasalia kuwa mwakilishi wa watu wa eneo la Kikuyu.

You can share this post!

2022: Ruto anavyotumia chakula cha msaada kujitangaza...

Mwanahabari wa K24 apatikana amefariki Molo

adminleo