• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 2:13 PM
Wanasoka wa KPL kupokea Sh10,000 kila mmoja kila mwezi kutoka kwa serikali kipindi hiki kigumu

Wanasoka wa KPL kupokea Sh10,000 kila mmoja kila mwezi kutoka kwa serikali kipindi hiki kigumu

Na CHRIS ADUNGO

WAZIRI wa Michezo, Amina Mohamed, amethibitisha kwamba wachezaji wa Ligi Kuu ya Soka ya Kenya (KPL) watakuwa wakipokezwa kiasi cha Sh10,000 kila mmoja kila mwezi kwa kipindi cha miezi mitatu ijayo.

Fedha hizo zinazonuia kuwapiga jeki wakati huu wa janga la corona ni sehemu ya mgao wa Sh20 milioni kutoka kwa Hazina ya Kitaifa ya Michezo.

Maagano ya kutolewa kwa fedha hizo yaliafikiwa wiki chache zilizopita kwa azma ya kuwasaidia wachezaji ambao wamekuwa wakikabiliana na hali ngumu ya kimaisha baada ya michezo iliyokuwa kitega-uchumi kwao kuahirishwa kwa sababu ya corona.

Kwa mujibu wa Amina, ni wachezaji na maafisa watano wa benchi za kiufundi kutoka kwa vikosi 12 husika vya KPL ndio wa pekee watakaonufaika kutokana na mgao huo.

“Tutatoa Sh10,000 kwa mwezi kwa kila mmojawapo wa wachezaji 30 na maafisa watano wa klabu 12 za KPL ambazo zimeathiriwa zaidi. Hii ina maana kwamba watakaofaidika ni jumla ya watu 420,” akatanguliza Amina.

“Mgao huu kutoka kwa Hazina ya Spoti utatolewa kwa kipindi cha miezi miwili ijayo huku kukiwepo uwezekano wa kuongezwa kwa mwezi wa tatu iwapo tutafaulu kupata fedha za ziada kutoka kwa wahisani na washirika wetu wa karibu,” akaongeza.

Kundi la kwanza la wachezaji wanaolengwa kunufaika na mradi huo wa serikali ni masogora wa Ligi Kuu ya KPL kabla ya msaada huo kuelekezwa kwa wanadimba wanaoshiriki ligi za madaraja ya chini katika soka ya humu nchini.

“Tumeafikiana kwamba tutaanza na KPL kwa sababu tunafahamu ugumu wa hali ambayo wachezaji wa kipute hicho wanapitia. Baada ya kutathmini orodha zote zilizowasilishwa na klabu husika, tumeandaa orodha ya mwisho ya wachezaji ambao wameathiriwa sana. Tutaanza nao huku tukiendelea kutathmini hali ilivyo katika kipindi cha siku 15 zijazo,” akasema.

Amina amesisitiza kwamba Wizara ya Michezo ina orodha ya mwisho iliyopigwa msasa licha ya baadhi ya klabu kuwasilisha idadi kubwa ya wachezaji kuliko ile iliyoagizwa.

Wanamichezo kutoka fani nyinginezo wanatarajiwa kuanza kunufaika kutokana na mgao huo wa jumla ya Sh50 milioni kutoka Hazina ya Spoti.

Amina aliwahakikishia wanaspoti wote wa humu nchini kwamba serikali itasimama nao katika hali zote katika kipindi hiki kigumu ambapo shughuli zote za michezo, ambazo ni kitega-uchumi kwa familia nyingi, zimesimamishwa.

“Nawahakikishia wanamichezo wetu kwamba hatujawasahau. Tunajitahidi kadri ya uwezo wetu kubuni njia zitakazowawezesha kujikimu kimaisha. Serikali inafahamu ugumu mnaopitia katika kipindi hiki ambapo njia zenu za pekee za kujitafutia riziki zimeathiriwa pakubwa na ugonjwa huu hatari.”

“Tumejitolea kwa hali zote kuwafaa mabalozi hawa wa taifa letu ambao ukawaida wa maisha yao umetikiswa zaidi na janga hili. Tumepania kuwapa msaada hadi corona itakapodhibitiwa vilivyo,” akaongeza.

You can share this post!

COVID-19: Ubalozi wa Iran na washirika wazindua jukwaa la...

SIHA NA LISHE: Karafuu na faida zake

adminleo