• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 1:15 PM
MABADILIKO: Timu ya KCB iliyotikisa bara Afrika kabla ya kufifia

MABADILIKO: Timu ya KCB iliyotikisa bara Afrika kabla ya kufifia

Na GEOFFREY ANENE

NI miaka 14 tangu KCB iduwaze Bara Afrika kwa kuibuka malkia wa mashindano ya klabu baada ya kunyamazisha miamba Al Ahly kutoka Misri kwa seti 3-2 katika fainali kali mjini Vacaos nchini Mauritius.

Timu hiyo ya benki ya KCB haikuwa imepata ufanisi kama huo tangu ianzishwe mwaka 1984 na pia haijawahi kuushuhudia tena.

Iliposhinda ubingwa wa Afrika 2006, ilikuwa chini ya kocha Paul Bitok, ambaye miaka miwili baadaye alinyakuliwa na Rwanda.

Wanabenki hao hawajawahi kushinda Ligi Kuu katika historia yao, ingawa wameng’ara mara kadhaa katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati.

Mwandishi huyu alitafuta kikosi cha KCB cha mwaka 2006 kufahamu kiko wapi na kinajishughulisha na nini.

Baada ya kuwa nchini Rwanda kukuza voliboli nchini humo kwa zaidi ya miaka 10, Bitok alirejea nyumbani na sasa ameajiriwa na timu hiyo kuwa mshauri wa kiufundi.

Kwa miaka miwili mfululizo, KCB imefanya usajili mkubwa wa wachezai na hata makocha ikitumai kutikisa ligini na pia kuwa namba wani barani Afrika.

Wachezaji waliofanyia kazi KCB mwaka 2006 ni Doris Palanga, Edinah Rotich, Sarah Chepchumba, Anastasia Macharia, Doris Muyeko, Rodah Liyali, Halima Bakari, Judith Tarus, Jackline Barasa, Mercy Moim, Esther Munyasia na Oba Okumu.

Palanga aliaga dunia. Mshambuliaji wa pembeni kushoto Rotich,39, anafanya kazi na jeshi la Kenya (KDF) sawa na Barasa,39, ambaye alikuwa mchezaji wa kati. Wote wawili walistaafu. Wamefanya kozi ya ukocha ya voliboli, ingawa hawajapata klabu. Enzi zao kama wachezaji walifahamika kwa makombora makali. Chepchumba, ambaye pia alicheza pembeni kushoto, anafanya kazi katika idara ya magereza baada ya kustaafu.

Macharia, ambaye alicheza pembeni kulia, alistaafu uchezaji. Aliolewa na refa mahiri wa voliboli Ismail Chege, ambaye pia ni afisa katika Shirikisho la Voliboli Kenya (KVF). Muyeko anaaminika kuwa katika maeneo ya Kawangware ama magharibi mwa nchi baada ya kuacha kucheza.

Lyali, 43, na Halima, ambao walikuwa maseta wa timu hiyo, pia sasa si wachezaji. Lyali anafanya kazi na kampuni ya Kenya Pipeline naye Halima ni mkufunzi wa timu ya voliboli ya wanawake ya Chuo Kikuu cha Mount Kenya.

Munyasia na raia wa Japan, Oba, ambao walicheza katika safu ya kati, waliyoyomea nchini Amerika na Japan mtawalia baada ya kustaafu. Oba aliyeolewa na kocha Mkenya Godfrey Owese Okumu anayeishi Japan, alipata idhini ya kuchezea KCB wiki chache tu kabla ya timu hiyo kuelekea Mauritius mwaka 2006.

Kutoka kikosi kilichoonyesha timu zingine za Afrika kivumbi mwaka 2006, Tarus na Moim ndio bado wanacheza. Wawili hawa walikuwa katika orodha ya wachezaji wengi waliogura KCB miezi sita baada ya mafanikio ya Mauritius.

Tangu mwaka 2007, Moim, 31,na Tarus,33, wamekuwa katika timu ya magereza (Kenya Prisons), ingawa Moim pia alichezea Liiga Ploki (Finland), Oriveden Ponnistus (Finland), Azerrail Baku (Azerbaijan) na Supreme (Thailand) kabla ya kurejea KCB mwezi Januari 2020. Moim sasa ndiye nahodha wa timu ya taifa ya Kenya almaarufu Malkia Strikers.

You can share this post!

COVID-19: Kenya yarekodi idadi ya juu zaidi ya visa vipya...

Muthama amkashifu Raila kuhusu kura ya maamuzi

adminleo