Habari

COVID-19: Visa 147 vipya, wote ni Wakenya

May 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

KENYA sasa imerekodi jumla ya visa 1,618 vya Covid-19 tangu iliporipoti kisa cha kwanza, baada ya wagonjwa 147 zaidi kuthibitishwa Alhamisi.

Idadi hiyo imebainika kutoka kwa sampuli 2,831 zilizochukuliwa zikafanyiwa vipimo katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema kati ya wagonjwa hao, 87 ni wanaume, jambo linaloendelea kusababisha taharuki kufuatia ongezeko la maambukizi ya Covid-19 miongoni mwa watu wa jinsia ya kiume.

Mgonjwa mwenye umri wa chini zaidi amekuwa mtoto wa umri wa mwaka mmoja huku wa juu akiwa na umri wa miaka 87.

“Wagonjwa wote leo Alhamisi ni Wakenya,” Waziri Kagwe amesema.

Amehimiza raia kutilia mkazo mikakati iliyowekwa kuzuia msambao wa corona.

Kaunti ya Nairobi inaendelea kuongoza kwa maambukizi, mtaa wa Kibra ukitajwa kuwa na wagonjwa 35 waliothibitishwa kwa muda wa saa 24 zilizopita. Nairobi imefuatwa na Kaunti ya Mombasa.

Wakati huo huo, wagonjwa watatu wamefariki idadi jumla ya walioaga dunia kutokana na Covid-19 ikifika wahanga 58.

Waziri Kagwe amefafanua kwamba waliofariki ni mmoja kutoka Thika, Kiambu na wawili wa Mombasa.

Aidha, wagonjwa 13 wamepona, idadi jumla ya waliopona kabisa ikifika 421.

Gavana wa Kaunti ya Kiambu – ambako ripoti ya Alhamisi imetangazwa – James Nyoro, amesema Soko Mjinga ni mojawapo ya maeneo hatari katika maambukizi ya Covid-19 Kaunti ya Kiambu. Sababu amesema ni idadi kubwa ya watu wanaozuru soko hilo.

Bw Nyoro amedokeza kwamba soko hilo linapokea wateja kutoka kaunti mbalimbali, ikiwemo Mombasa na pia wafanyabiashara kutoka nje ya nchi.

“Tumelifunga kwa muda ili kutekeleza shughuli ya kunyunyuzia dawa,” gavana amesema.

Maeneo mengine hatari katika maambukizi ya Covid-19 Kiambu kutokana na idadi kubwa ya watu ni pamoja na soko la Makongeni, Githurai, Ngewa, Kiambu Mjini na maeneo yanayopakana na mji huo.

Alhamisi gavana Nyoro amesema kufikia sasa kaunti hiyo imefanya vipimo vya watu 509 ambapo 37 wamepatikana na ugonjwa wa Covid-19.

Aidha, serikali yake imeajiri wahudumu 200 wa afya, akiahidi 100 zaidi kuajiriwa kufikia wiki ijayo.

“Tunahitaji kufanya vipimo zaidi na tunaomba serikali kuu itufadhili na vifaa vingi vya shughuli hii,” gavana akarai.

Dkt Nyoro amesema hayo baada ya kukutana na Kagwe katika makao makuu ya kaunti hiyo, Kiambu.

Waziri Kagwe naye pia alikuwa ameandamana na mwenzake wa Teknolojia na Mawasiliano (ICT) Joe Mucheru.