• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
EPL kurejelewa Juni 17

EPL kurejelewa Juni 17

Na CHRIS ADUNGO

KAMPENI za Ligi Kuu ya Uinegreza (EPL) sasa zitarejelewa Juni 17, 2020, kwa mechi mbili zitakazokutanisha Aston Villa na Sheffield United kisha Manchester City na Arsenal.

Mechi hizo ni zile zilizokuwa zimesalia kwa vikosi hivyo kucheza ili kufikia idadi ya michuano 29 ambayo wapinzani wote wengine 16 walikuwa wamepiga hadi kipute hicho kiliposimamishwa kwa muda kutokana na janga la corona mwanzoni mwa Machi 2020.

Mechi zote za raundi nzima ya 30 zimeratibiwa kusakatwa kati ya Ijumaa ya Juni 19 na Jumapili ya Juni 21, 2020.

Vikosi vyote 20 vya EPL vinatarajiwa kulijadili zaidi pendekezo hilo katika kikao cha leo usiku japo wadau wote wameafikiana kuhusiana na mipango hiyo iliyopo hadi kufikia hatua ya sasa.

Hadi kampeni za EPL zilipoahirishwa, zilikuwa zimesalia jumla ya mechi 92 za kutandazwa muhula huu.

Kipute cha EPL kilisimamishwa mnamo Machi 13 na itarejelewa siku 100 tangu Leicester City walipowanyuka Villa 4-0 mnamo Machi 9, 2020.

Mechi zote zilizosalia zitasakatiwa ndani ya viwanja vitupu bila mahudhurio ya mashabiki.

Mnamo Jumatano, vikosi vya EPL vilipiga kura ya pamoja na kuafikiana kuhusu pendekezo la kuwaruhusu wachezaji kushiriki mazoezi kwa kukabiliana kwa karibu tangu warejee kambini yapata wiki moja iliyopita kwa minajili ya kujifua kwa mechi zilizosalia.

Hadi kufikia sasa, visa 12 vya maambukizi ya virusi vya corona vimeripotiwa miongoni mwa vikosi vya EPL baada ya jumla ya watu 2,752 kupimwa.

Wachezaji wa EPL pamoja na maafisa wa vikosi vinavyoshiriki kivumbi hicho wataendelea kupimwa mara mbili kwa wiki huku kila kikosi kikiongezewa kiwango cha kupima hadi watu 60 kwa siku kutoka kwa 50 waliokuwa wakiweza kufanyia vipimo wiki nne zilizopita.

Mchezaji au afisa yeyote atakayepatikana na virusi vya corona atatengwa au kutiwa katika karantini kwa kipindi cha siku saba huku hali yake ikitathminiwa kwa karibu na maafisa wa afya.

Hatua ijayo katika juhudi za kurejelewa kwa kampeni za EPL ni kuwaruhusu wachezaji waanze kushiriki mazoezi ya kawaida katika kambi zao mbalimbali huku suala la kuteua viwanja vitakavyotumiwa kwa mechi hizo zilizosalia likijadiliwa zaidi kuanzia kesho Ijumaa.

Kufikia sasa, Liverpool wanaopigiwa upatu wa kutwaa ubingwa wa EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 82. Pengo la pointi 25 linatamalaki kati yao na mabingwa watetezi Man-City ambao ni wa pili jedwalini.

Bournemouth, Aston Villa na Norwich City wapo katika hatari ya kuteremshwa ngazi hasa ikizingatiwa kwamba wanakokota nanga mkiani kwa alama 27, 25 na 21 mtawalia.

You can share this post!

Hatima ya Jumwa, Wamalwa yaamuliwa

Mishi Mboko ashukuru kuchaguliwa mwanachama wa tume ya...

adminleo