Kipenga cha kuashiria kurejelewa kwa Serie A kupulizwa rasmi Juni 20
Na CHRIS ADUNGO
KIVUMBI cha Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kitarejelewa mnamo Juni 20, 2020.
Haya ni kwa mujibu wa Waziri wa Michezo nchini Italia, Vincenzo Spadafora.
Kampeni za Serie A ziliahirishwa mnamo Machi 9, 2020, zikiwa zimesalia raundi 12 za mechi za kusakatwa kabla ya msimu huu kutamatika rasmi. Hadi kufikia wakati huo, mabingwa watetezi Juventus walikuwa wakiselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 63, moja zaidi kuliko Lazio ambao wanashikilia nafasi ya pili.
Wachezaji wa Serie A walianza mazoezi ya kila mmoja kivyake mwanzoni mwa Mei 2020 kabla ya kuruhusiwa kushiriki mazoezi katika makundi madogo ya watu watano mwanzoni mwa wiki hii.
Mnamo Mei 20, Shirikisho la Soka la Italia (FIGC) lilisisitiza tarehe 20 Agosti, 2020 kuwa siku ya mwisho kwa kampeni zote za Serie A katika msimu huu wa 2019-20 kutamatika rasmi kabla ya muhula ujao wa 2020-21 kuanza Septemba 1, 2020.
FIGC ilishikilia kwamba ni matarajio yake kushuhudia ligi za madaraja matatu ya kwanza nchini Italia zikifikia tamati msimu huu. Ingawa hivyo, vinara wa shirikisho hilo walifichua uwezekano wa mchujo kutumika kuamua washindi wa kila ligi iwapo vipute vyote vitalazimika tena kusitishwa pindi baada ya kurejelewa.
Licha ya baadhi ya vinara wa klabu za Serie A kushikilia kwamba wapo tayari kwa kivumbi hicho kurejelewa hata Juni 13, Massimo Cellino ambaye ni mmiliki wa kikosi cha Brescia kinachokokota nanga mkiani mwa jedwali amepinga vikali mapendekezo ya kuanza upya kwa soka ya Italia kabla ya janga la corona kudhibitiwa vilivyo.
“Kurejelewa kwa Serie A ni mzigo mkubwa kwa wachezaji. Tuliacha kushiriki mazoezi mazito miezi miwili iliyopita. Ni hatari sana kuanza ghafla kusakata mechi tatu kwa wiki. Nahofia kwamba tutakuwa na visa vingi vya majeraha hasa ikizingatiwa joto jingi linaloshuhudiwa kwa sasa nchini Italia,” akasema Cellino.
Msimamo wa Cellino unatofuatiana na ule wa beki matata wa Udinese na timu ya taifa ya Nigeria, William Troost-Ekong anayeamini kwamba kurejelewa kwa Serie A kutaamsha hamasa zaidi miongoni mwa wachezaji na kurejesha wingu la matumaini miongoni mwa wakazi wa Italia.