• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 10:55 AM
Ngome kuu ya Ruto yajuta kuingiza URP katika Jubilee

Ngome kuu ya Ruto yajuta kuingiza URP katika Jubilee

Na WAANDISHI WETU

VIONGOZI wa kisiasa katika ngome ya Naibu Rais William Ruto eneo la Rift Valley, wameanza kujutia uamuzi wao kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta.

Eneo la Rift Valley lilikuwa miongoni mwa yale ambayo yalivunja vyama ili kuunda Jubilee.

Miongoni mwa vyama vilivyovunjwa ni kile cha URP kilichoongozwa na Dkt Ruto.

Endapo Jubilee itasambaratika ifikapo 2022, huenda viongozi wa eneo hilo wakawa taabani kisiasa.

Wanasiasa hao wanaojumuisha wabunge, magavana na viongozi wa kijamii wamedai hatua zinazochukuliwa katika Jubilee kuadhibu wafuasi wa Dkt Ruto, ni ishara tosha kuwa Rais Kenyatta anaipa jamii ya eneo hilo asante ya punda.

Hii ni licha ya kuwa Rais amejitokeza kusema uamuzi wa kufanya mabadiliko ya uongozi chamani ni kwa lengo la kutimiza ajenda zake kwa wananchi.

Mbunge wa Kapenguria Samuel Moroto, alisema si haki watu kuadhibiwa kwa msingi wa misimamo yao chamani, na endapo wamekosea, ni sharti sheria zifuatwe kuwaadhibu.

“Huu muhula wa mwisho Rais anataka kumaliza vibaya. Bwana Rais kile unafanya hakitatusadia. Tulijua kuwa wakati Rais Uhuru anamaliza kipindi chake, Ruto anachukua usukani,” akasema Bw Moroto.

Mbunge wa Kacheliba Mark Lomunokol naye alisema sasa watu wanajionea wazi athari za kukubali vyama vyao kuvunjwa.

“Nilifurushwa kutoka Jubilee kupitia kwa simu kabla ya mchujo wa 2017. Inaonekana Rais analenga kuunda tena miungano na vyama vingine. Kwa sasa niko chama cha PDR na sitakubali kujumuishwa kwenye muungano wa Jubilee,” akasema.

Wengine walisema uaminifu wa jamii za Rift Valley kwa Rais Kenyatta ulianza zamani, kwa hivyo inashangaza anawasaliti.

Gavana wa Nandi Stephen Sang na Mbunge wa Chesumei Dkt Wilson Kogo, walitoa mfano wa wakati aliyekuwa mbunge maalum Mark Too alipojitolea kujiuzulu ili kumwezesha Rais Kenyatta kuingia bungeni, kisha baadaye akawania urais 2002.

“Jamii ya Wakalenjin imemuunga mkono Rais tangu 2002. Jamii hii inafaa kuheshimiwa chamani,” akasema.

Walipuuzilia mbali misimamo ya wakuu wa Jubilee kwamba chama kinatekeleza nidhamu na kusisitiza kuwa nia ya mabadiliko yanayofanywa ni kumchapa kiboko Naibu Rais.

“Tuna wasiwasi sana na yale yanayoendelea katika Jubilee. Tulimuunga mkono Rais kwa idadi kubwa mno ya wapigakura, lakini sasa inaonekana ametusahau,” akasema Bw Kogo.

Hata hivyo, walisisitiza wataendelea kukaa Jubilkee hadi mwisho, na njama zinazoendelezwa hazitafaulu.

Vyama vingine vilivyovunjwa kuunda Jubilee ni TNA, Grand National Unity (GNU), Alliance Party of Kenya (APK), The Independent Party (TIP), New Ford Kenya, Ford-People, Jubilee Alliance Party (JAP), United Party of Kenya (UPK) na The Republican Congress (RC).

Viongozi wengine wa vyama vilivyovunjwa kama vile aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri, aliyeongoza GNU na Kalembe Ndile (TIP) pia hulalamika kusalitiwa.

Bw Kiunjuri tayari ashabuni chama kipya cha The Service Party (TSP) anachosema kuwa “kitaleta msisimko mpya katika siasa za Kenya.”

 

Ripoti za Oscar Kakai, Wycliffe Kipsang, Tom Matoke na Wanderi Kamau

You can share this post!

Serikali yaambia wazazi walipe karo hata kama shule...

KAMAU: Inasikitisha kuona waliopigania demokrasia...

adminleo