• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Wetang’ula alaumu Atwoli kwa masaibu yake

Wetang’ula alaumu Atwoli kwa masaibu yake

Na IBRAHIM ORUKO

SENETA wa Bungoma Moses Wetang’ula, amemlaumu Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli kwa madai ya kuchochea kung’atuliwa kwake kama kinara wa chama cha Ford-Kenya.

Bw Wetang’ula, ambaye alijitokeza baada ya kuondolewa kwake na Baraza Kuu la chama (NEC), alisema mipango ya kumtimua ilifanyika katika mkutano wa viongozi wa eneo la Magharibi nyumbani kwa Bw Atwoli katika Kaunti ya Kajiado.

“Hauhitaji kuwa mwanasayansi kujua kuwa kilichofanyika leo kilipangwa Ijumaa eneo la Kajiado. Hauwezi kuchagulia jamii viongozi,” akasema Bw Wetang’ula.

Hata hivyo, Bw Atwoli alipuuzilia mbali madai hayo akimtaja seneta huyo wa Bungoma kuwa mtu asiye na maendeleo, na ambaye anapenda kulalamika.

“Mkutano ambao ulimuinua Bw Musalia Mudavadi kuwa uongozi wa jamii ya Waluhya 2016 ulianzia kwa nyumba hii yangu,” alisema Bw Atwoli akizungumzia msururu wa mikutano ambayo iliishia na kutawazwa kwa kiongozi wa chama cha ANC kama msemaji wa jamii hiyo mnamo Disemba 2016 katika uwanja wa Bukhungu.

“Nakumbuka Bw Wetang’ula alikataa kuhusika na mikutano na pia alikosa kufika mkutano wa Bukhungu. Alikuwa ananishtumu kwa kumtumia Bw Mudavadi kumhujumu,” alisema Bw Atwoli.

Vita hivi vya maneno vilichipuka baadhi ya wanachama wa kamati kuu ya Ford Kenya walipopiga kura kumuondoa Bw Wetang’ula na Katibu Mtendaji Bw Chris Mandu Mandu kwa madai ya ukiukaji mkubwa wa katiba, sheria na maadili.

Seneta huyo pia anashtumiwa kwa kuingilia taratibu za mchujo wa chama mnamo 2017 ambazo inadaiwa ziligharimu chama nafasi bungeni pamoja na kukosa kupatanisha pande zilizokuwa zikizozana.

Jana, Mbunge wa Kanduyi, Wafula Wamunyinyi alichaguliwa kuchukua nafasi ya Bw Wetang’ula kama kaimu, Bi Josephine Maundu akishikilia cheo cha kaimu katibu mtendaji.

Akipinga mabadiliko hayo, Bw Wetang’ula alionekana kuhisi kusalitiwa na wale aliowataja kuwa marafiki wake wa karibu na kutangaza pia kuwang’oa katika nafasi walizoshikilia.

Alisema nafasi ya Dkt Eseli Simiyu ambaye ni katibu mkuu wa chama, itashikiliwa na mbunge wa Kiminini, Chris Wamalwa, na ya Wamunyinyi kuchukuliwa na mbunge wa West Mugirango, Vincent Mogaka.

“Bw Wamunyinyi amekuwa akitembea kwa kivuli changu kwani mimi ndiye nilimteua kuwa mjumbe maalum wa Kenya nchini Somalia,” alieleza.

Baadhi ya waliohudhuria mkutano wa NEC ni pamoja na Dkt Simiyu, mbunge wa Kisumu Magharibi Olago Oluoch, Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati na aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la wazee wa jamii ya Waluhya Patrick Wangamati.

“Tulichukua uamuzi huu kwa kuwa tunataka kuwa sehemu ya mipangilio ya kisiasa katika ngazi ya kitaifa. Tunaunga utaratibu wa BBI na handisheki,” alisema Bw Wangamati akipuuza madai kuwa walipanga mapinduzi hayo katika mkutano wa Kajiado mnamo Ijumaa.

Pia alisisitiza kuwa kuondolewa kwa Bw Wetang’ula hakuna uhusiano wowote na dhana kuwa yuko karibu na Naibu Rais William Ruto.

You can share this post!

Bei ya unga kushuka mahindi ya Mexico yakifika

Nitakwama na Ruto hata mkinipokonya cheo – Washiali

adminleo