Habari Mseto

Tufikirie upya malengo yetu – Rais Kenyatta

June 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 3

NA PSCU 

Rais Uhuru Kenyatta Jumatatu amesema wakati umefika kwa Kenya kuanza kufikiria upya maono ya kiuchumi na kisiasa kuliandaa taifa kwa maendeleo makubwa zaidi.

Akilinganisha hali ya Kenya na ile inayosimuliwa katika Biblia, Rais alisema Kenya kwa sasa iko na zaidi ya miaka 50, na kitabu hicho kitakatifu kilihitaji mataifa kuweka mwanzo mpya kila baada ya miaka 50.

Alisema matendo ambayo watu waliyaita “mwaka wa Yubili” yalileta mabadiliko ya moyo; uponyaji kwa taifa na mitazamo mipya kwa watu wake.

Kiongozi wa taifa alizungumza katika Ikulu ya Nairobi, alipoongoza taifa kuadhimisha sherehe za miaka 57 za Sikukuu ya Madaraka. Awali hafla hiyo ilikuwa iandaliwe huko Kisii lakini kutokana na kanuni za usafiri zilizowekwa kukabili kuenea kwa janga la Covid-19, ilifanyika Jijini Nairobi.

Kuhusu siasa, Rais alisikitikia hali ya migawanyiko ya siasa nchini na akapigia debe kupangwa upya kwa mfumo wa kisiasa nchini.

“Iwapo tumetekeleza mambo makubwa katika suala la ujenzi, mambo makubwa zaidi yaliyosalia ni kuhusu mfumo wetu wa uongozi,” kasema Rais.

Kiongozi wa Taifa aliwashauri Wakenya kutohofia kubadilisha mfumo wa kisiasa nchini akisema mfumo huo haushughulikii malengo ya sasa na ya baadaye.

“Hatuwezi kufikiria upya utaifa wetu bila kubadilisha mfumo wetu wa kisiasa. Na hatuwezi kubadilisha mfumo huu bila kubadilisha upya katiba yetu,” kasema Rais.

Alisema azma yake ni kuboresha katiba “na kusuluhisha tulichokosea mwaka wa 2010.”

Alisema: “Kipindi cha kikatiba ninacho azimia ni kile ambacho kitamaliza msururu wa vurugu ambazo tumeshuhudia kila baada ya uchaguzi mkuu tangu mwaka 1992.”

Mbali na siasa, Rais alisema Kenya pia inahitaji mabadiliko ya utamaduni yake ya uraia.

“Iwapo tutaleta mwanzo mpya na kufikiria upya maono yetu kama taifa, sharti tubadilishe desturi zetu za uraia na tupate ule ambao unazingatia majukumu, bidii na maadili mema,” kasema Rais

Kuhusu uchumi, Rais Kenyatta alisema serikali yake imeafikia mafanikio makubwa katika kutimiza Ruwaza ya Maendeleo ya mwaka 2030 kupitia utekelezaji wa Nguzo Nne za Ajenda Kuu ya Maendeleo.

Alisema Ruwaza ya Maendeleo ya 2030 itakamilika miaka 9 ijayo na kusema kwamba kuna haja ya dharura ya kubuni ruwaza nyingine na maono mapya.

Akitoa mfano wa uekezaji wa serikali yake kwenye muundomsingi, mabadiliko katika elimu, mafunzo ya kiufundi, kusambazwa kwa umeme pamoja na afya bora, Rais alisema ajenda ya mabadiliko ya serikali ilitokana na maono ya pamoja ya viongozi waanzilishi.

“Serikali yangu imejenga barabara za umbali wa kilomita 1,000 za lami kila mwaka. Hii ni zaidi ya mara 44 ya zile barabara ambazo serikali ya kikoloni ilijenga, na zaidi ya mara 4 ya barabara zilizojengwa kwa jumla na serikali tatu za kwanza kila mwaka,” kasema Rais.

Vile vile, Rais Kenyatta aligusia maendeleo na upanuzi wa bandari kama malango ya kuingia kwenye masoko ya eneo hili pamoja na yale kimataifa.

Huku kukiwa na ujenzi wa bandari mpya ya Lamu pamoja na kufufuliwa kwa bandari ya Kisumu kunakoendelea, Rais alisema serikali itaendelea kuekeza katika miradi ya kuboresha muundomsingi.

Mbali na reli ya kisasa ya SGR ambayo tayari inahudumu kati ya Mombasa na Naivasha, Rais alisema serikali yake inasimamia ufufuzi wa laini za zamani za reli.

“Mbali na reli ya kisasa ya SGR, nafufua reli kati ya Nairobi na Nanyuki inayopitia kaunti 6. Ufufuzi wa reli ya zamani kati ya Naivasha hadi Malaba uko karibu kuanza.”

Rais alisema serikali inaendelea kutekeleza marekebisho katika sekta ya elimu nchini hususan mafunzo ya kiufundi na anuai ili kuimarisha nguvu kazi katika uchumi unaobadilika ulimwenguni.

Kiongozi wa Taifa pia alizungumzia kwa kina kuhusu mafanikio makubwa katika usambazaji wa stima akisema chini uongozi wake wa miaka 7, nyumba milioni 3.5 mpya zimewekewa stima ikilinganishwa na nyumba milioni 4.5 zilizonakiliwa enzi ya ukoloni hadi mwaka 2013.

“Hii inamaanisha kwamba tumefanya kazi zaidi mara 15 ikilinganishwa na serikali za awali katika kuwawekea watu wetu stima,” kasema Rais katika sherehe iliyopeperushwa kwa njia ya runinga na pia kuhudhuriwa na Naibu Rais Dkt William Ruto na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana nchini Wycliffe Oparanya ambaye pia ni Gavana wa kaunti ya Kakamega.

Kuhusu afya, Rais alisema serikali yake imo mbioni kutekeleza Mpango wa Utoaji Huduma za Afya bora kwa Wote akiongeza kwamba kila kaunti sasa iko na vifaa vya kisasa vya afya.

Akizungumza kifupi kuhusu mikakati ya sasa ya kukabili janga la Covid-19, Rais alisema serikali inafanya mashauriano na viongozi wa kidini pamoja na washikadau katika sekta ya elimu kuhusu hatua zinazostahili kuchukuliwa.

Naibu Rais Ruto alisema janga la Covid-19 limeathiri wakenya pakubwa na kubadilisha mienendo ya maisha.

Alisema kwamba huku shule zikiwa zimefungwa, maeneo ya kuabudia yakiwa yamefungwa na wengi kupoteza kazi, maisha yamekuwa magumu kwa wengi.

Naibu Rais alitoa wito kwa kila mkenya kuunga mkono mikakati inayotekelezwa na serikali kukabili athari za janga la Covid-19.

Gavana Oparanya alimpongeza Rais kutokana na wajibu wake katika vita dhidi ya janga la Covid-19 akisema serikali ya kitaifa imeendelea kutoa rasilimali ambazo kaunti zinahitaji kukabili janga hilo.