Habari MsetoSiasa

Mapinduzi ya siasa ya Mudavadi, Weta yanukia Magharibi

June 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 3

LUCY KILALO na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa chama cha ANC Musalia Mudavadi na Seneta wa Bungoma, Moses Wetang’ula sasa wamejitokeza kumuonya Raila Odinga dhidi ya kugawanya jamii ya Mulembe.

Viongozi hao ambao walihutubia wanahabari jana wakiwa nyumbani kwa Bw Wetangula walimtaja Bw Odinga kama mgeni ambaye baada ya kukaribishwa vyema, anamgeuka mwenyeji wake.

“Inasikitisha kuwa baadhi ya wale ambao tumeunga mkono wanafikiria kuwa sisi ni punda. Wanadhani wanaweza kututumia kufika wanakotaka na baada ya kufika, wanatutupa na kututusi. Tumeona hili hasa kwa upande wa uongozi wa ODM chini ya Raila Odinga. Kushinda yeyote mwingine, Odinga amenufaika na nia njema ya watu wa Magharibi,” taarifa iliyotiwa saini na viongozi 21, saba wakiomba udhuru, ilisema.

Iliongeza, “Tumemruhusu mara kadhaa kuwa mwaniaji wa urais, hata wakati ambapo tulijua kuwa tuna wagombea bora zaidi. Tulimchukua kama ndugu mpendwa tuliyemthamini. Lakini amefanya nini? Amejiendesha kama mgeni mjeuri, na ameenda kila sehemu ya nyumba, pamoja na maeneo ambayo ni mwiko kufika. Amehimiza watoto kuwa wajeuri kwa wakubwa wao. Ameshawishi kuwatusi wazazi wao.”

Wakati huo huo, walisema kuwa Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli, Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya na Waziri Eugene Wamalwa, hawawezi kuongea kwa niaba ya Waluhya.

“Haijalishi umepanda na kufikia nafasi gani kwa sababu ya nia njema ya watu wetu, tunakutahadharisha usifikirie kuwa unaweza kuongea kwa niaba yetu bila idhini yetu,” walisema kupitia taarifa hiyo iliyosomwa na mbunge wa Kiminini, Dkt Chris Wamalwa.

Waliohudhuria mkutano wa jana ni pamoja na wabunge Ben Washiali, Justus Murunga, Didymus Baraza, Ferdinand Wanyonyi, Tindi Mwale miongoni mwa wengine.

Aidha, mapinduzi ya kisiasa yanawaandama, kiongozi wa chama cha ANC, Bw Mudavadi na mwenzake wa Ford-Kenya, Bw Moses Wetangula, kama vigogo wakuu wa siasa katika jamii ya Abaluhya. Wawili hao ndio wamekuwa wakionekana kuwa wawakilishi na wasemaji wakuu kisiasa wa jamii hiyo, huku sauti zao zikiamua mwelekeo ambao jamii hiyo huchukua.

Hata hivyo, hatua ya baadhi ya wanachama wa Baraza Kuu (NEC) la Ford-Kenya kumng’oa mamlakani Bw Wetang’ula, ambaye pia ndiye Seneta wa Bungoma kama kiongozi wa chama mnamo Jumatatu, imeanza mchakato ambao wadadisi wa siasa wametaja kuwa “mapinduzi” ya kisiasa ya wawili hao katika jamii ya Mulembe.

Kwenye kikao kilichoongozwa na Katibu Mkuu wa chama, Dkt Eseli Simiyu, baraza hilo lilimng’oa mamlakani Bw Wetang’ula na kumchagua mbunge Wafula Wamunyinyi (Kanduyi) kama kaimu kiongozi.

Kikao pia kiliidhinisha kutolewa kwa Bw Chris Mandu kama Katibu Mashirikishi.

Hata hivyo, Bw Wetang’ula “alimjibu” Dkt Simiyu kwa kumtoa kama Katibu Mkuu na nafasi yake kuchukuliwa na mbunge wa Kiminini, Dkt Chris Wamalwa.

Lakini muda mfupi baadaye, Bw Mudavadi alitoa taarifa kali, akimlaumu mojawapo ya viongozi wa muungano wa Nasa kwa kupanga njama za kusambaratisha vyama tanzu kwenye muungano huo.

Na ingawa hakumtaja moja kwa moja, taarifa ya Bw Mudavadi ilimlenga kinara wa ODM, Bw Raila Odinga, hali iliyokifanya chama hicho kutoa jibu kali kwa Bw Mudavadi, iliyomtaja kama mwanasiasa ambaye hutegemea kuungwa mkono.

“Bw Mudavadi ni kiongozi ambaye daima amekuwa akitegemea kufaidika kwa kuungwa mkono na miungano ya kisiasa inayobuniwa. Lazima afahamu kujijenga,” ikasema ODM, kupitia Katibu Mkuu Edwin Sifuna. Kutokana na majibizano hayo, wadasisi wa siasa wanataja mwelekeo huo kama ishara ya mikakati ya wanasiasa wakuu nchini “kung’ang’ania” uongozi wa jamii ya Abaluhya.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo jana, mchanganuzi wa siasa, Bw Javas Bigambo, anasema kuwa mwelekeo huo unaashiria mwanzo wa mapambano makali ya kisiasa kati ya Bw Mudavadi, Bw Wetang’ula na wimbi la viongozi wapya wanaohisi kuwa wakati wao kuchukua uongozi wa jamii hiyo umetimia.

Kulingana na Bw Bigambo, wimbi hilo linawakilishwa na karibu viongozi 40 waliokutana na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli katika makazi yake, Kajiado, Jumamosi.

“Mapinduzi ya kisiasa dhidi ya Mabwana Mudavadi na Wetang’ula yanaongozwa kichinichini ya Bw Atwoli kwa kuwatumia viongozi wapya na wachanga, ili kuleta mwamko mpya wa kisiasa katika eneo la Magharibi,” asema, akiongeza kuwa imefikia wakati wabuni njia mwafaka za kisiasa kuhimili wimbi hilo.