• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
Vita vya Ford Kenya vyatua kwa Msajili wa Vyama

Vita vya Ford Kenya vyatua kwa Msajili wa Vyama

Na DAVID MWERE

VITA vya uongozi katika chama cha Ford Kenya huenda sasa vikaelekea kwa Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa.

Hii ni baada ya makundi pinzani kuwasilisha majina tofauti kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bi Anne Nderitu vikidai uongozi wa chama hicho.

Kundi linaloongozwa na Mbunge wa Kanduyi, Bw Wafula Wamunyinyi lilikuwa la kwanza katika afisi ya msajili kuonyesha kuwa mbunge huyo alikuwa amechaguliwa vilivyo kuchukua nafasi ya seneta wa Bungoma, Moses Wetang’ula kama kinara wa chama katika mkutano maalum wa Baraza Kuu la chama Jumapili.

Dakika chache baada ya kuondoka, kundi linaloegemea kwa Bw Wetang’ula liliwasilisha stakabadhi kuonyesha kuwa angali kinara wa chama.

Pia lilionyesha kuwa Bw Wamunyinyi na Katibu Mkuu, Dkt Eseli Simiyu ambaye ni mbunge wa Tongaren, walikuwa wamesimamishwa na chama, na kwa hivyo hawakuwa na idhini ya kuendesha shughuli zake.

Kundi la Bw Wetang’ula lilitangaza kuwa nafasi ya Bw Wamunyinyi ilikuwa imechukuliwa na mbunge wa Mugirango Magharibi, Bw Vincent Kemosi na kuwa Dkt Simiyu si katibu wake kwa kuwa mahali pake sasa pamechukuliwa na Dkt Chris Wamalwa wa Kiminini.

Macho sasa yako kwa afisi ya msajili wa vyama ambaye alisema kuwa atafanya uamuzi baada ya kukagua stakabadhi zilizowasilishwa.

“Tunaangalia stakabadhi kuona ikiwa zinaambatana na Sheria ya Vyama vya Kisiasa na Katiba ya Kenya,” alisema Bi Nderitu.

Katika vikao tofauti, makundi hayo yalitahadharishana kuhusu kuchukua hatua za kinidhamu iwapo wataendelea kukiuka katiba ya chama, Sheria ya Vyama vya Kisiasa na Katiba ya Kenya.

You can share this post!

Uhuru amtembeza Raila jijini usiku

Wanafunzi 2600 wakataa digrii, wajiunga na taasisi za...

adminleo