Habari Mseto

Polisi wageuka makuhani wa mauti wakati huu wa janga la corona

June 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

MARY WAMBUI na BENSON MATHEKA

FAMILIA ya Yassin Moyo ingali na majonzi tangu ilipompoteza mnamo Machi 31 baada ya kupigwa risasi tumboni na polisi wakitekeleza kafyu katika eneo la Kiamaiko, Huruma, Nairobi.

Ingawa wanahisi afueni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuagiza kukamatwa na kushtakiwa kwa Duncan Ndiema, afisa wa polisi katika kituo cha Huruma kwa dai la kufyatua risasi iliyokatiza maisha ya mwanao, majonzi yangalipo kwani maisha hayajakuwa rahisi tangu walipompoteza mtoto huyo.

“Fikira kuwa mtu aliyemuua mwanao yuko huru na humfahamu, ni jambo la kutia hofu. Angalau sasa mioyo yetu inaweza kutulia kidogo,” alisema babaye marehemu, Bw Hussein Moyo.

Tukio hilo ni miongoni mwa mengine mengi ambayo polisi wameshtumiwa kuyatekeleza katika sehemu tofauti nchini, hasa katika kipindi hiki cha janga la corona.

Katika kisa cha hivi punde, polisi wanadaiwa kumuua kwa kumpiga risasi mwanamume mzee asiye na makao walipompata nje usiku.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji, visa 80 vya ukatili wa polisi vimeripotiwa katika ofisi yake tangu Desemba mwaka jana. Watetezi wa haki za binadamu wanasema kwamba visa hivi vinazidi kuongezeka kwa sababu maafisa wanaohusika hawaadhibiwi.

“Ni nadra sana maafisa wa polisi wanaotumia nguvu kupita kiasi na kuua maskini kiholela kuadhibiwa. Hali hii imewapa nguvu za kuendeleza ukatili dhidi ya raia wanaopaswa kulinda,” asema mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch, Bw Otsiemo Nyamwaya. Bw Haji anasema ofisi yake inashirikiana na Mamlaka Huru ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA) kuchunguza visa vya ukatili unaotekelezwa na polisi.

“Tangu Oktoba 2019, ofisi yangu imepokea kesi 80 kuhusu ukatili wa polisi na inashirikiana na IPOA kuhakikisha kesi hizi zimeharakishwa,” alisema Bw Haji.

Mwenyekiti wa IPOA Anne Makori alithibitisha kuwa shirika hilo limepokea malalamishi 87 ya ukatili wa polisi tangu waanze kutekeleza kanuni za kuzuia corona Machi mwaka huu vikiwemo visa 15 vya mauaji ya kiholela ambavyo vinaendelea kuchunguzwa.

“Mamlaka hii imepokea malalamishi 87 ya ukatili wa polisi tangu Machi 27 2020. Malalamishi haya yanahusu mauaji, ufyatuliaji risasi, unyanyasaji, ubakaji na unyang’anyi,” Bi Makori alisema kwenye taarifa. Wanaharakati wanasema kesi nyingi za ukatili wa polisi hazifaulu baada ya washukiwa na maafisa wenzao kuwatisha mashahidi.

“Polisi wanaotekeleza ukatili dhidi ya raia wamekuwa wakiwatisha mashahidi na waathiriwa wanaonusurika. Kwa sababu hii, watu wengi wamekuwa wakikosa kupata haki. Hii inawapa maafisa hao nguvu ya kuendelea na ukatili wao,” asema Simon Kihoro, mtetezi wa haki katika mtaa wa Mathare, Nairobi.

Bw Kihoro anatilia shaka uwezo wa IPOA wa kuhakikisha polisi wanaokiuka haki za raia wanaadhibiwa akisema shirika hilo halina wafanyakazi wa kutosha. Kwa mujibu wa Bw Haji, IPOA inafanya kazi nzuri licha ya changamoto ya kukosa wafanyakazi wa kutosha.

Mnamo Januari 15, Stephen Muchurusi ,19 aliuawa katika maandamano katika mtaa wa Kasarani. Mwezi huo huo mtaani Majengo, maafisa wawili wa polisi waliokuwa kwenye doria walimuua kwa kumpiga risasi Ahmed Majid aliyekuwa na umri wa miaka 24.

Mnamo Januari 24, 2020, IPOA ilisema kwamba visa vya ukatili wa polisi vilikuwa vimeongezeka nchini na wanaharakati wanasema hali inazidi kuwa mbaya. Bi Makori alitaja mauaji ya Yassin, mzee aliyeuawa Mathare, watu wawili waliouawa kaunti ya Nandi, mwanamke aliyepigwa risasi na polisi eneo la Emali na mauaji ya watu watatu wa familia moja kaunti ya Kwale mnamo Mei 30 kuwa baadhi ya malalamishi ambayo IPOA inachunguza.

Msemaji wa polisi Charles Owino anakiri kwamba baadhi ya maafisa wa polisi wanakiuka haki za binadamu kwa kutumia nguvu kupita kiasi akisema wengi wao ni vijana wanaoweza kutumia mamlaka yao visivyo. Bw Owino anasema afisa yeyote atakayepatikana na hatia atachukuliwa hatua kali za kisheria.