• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Mahangaiko mitaani watu wakikosa kodi

Mahangaiko mitaani watu wakikosa kodi

Na SAMMY WAWERU

Visa vya malandilodi kubomolea wapangaji mapaa ya nyumba, kuwafungia milango na hata kuwafurusha kwa kulemewa kulipa kodi wakati huu janga la Covid – 19 linaendelea kuhangaisha ulimwengu vimeripotiwa.

Aghalabu, ni matukio yanayoendelea kushuhudiwa maeneo ya mijini, kaunti ya Nairobi ikiongoza katika visa hivyo.

Ugonjwa wa Covid – 19 ambao sasa ni janga la kimataifa, umeathiri uchumi wa mataifa kwa kiasi kikuu, ikiwemo sekta mbalimbali na kusababisha watu kupoteza nafasi za kazi.

Huku maambukizi yakiendelea kuongezeka kila uchao, athari za homa hii ya corona zinazidi kuongezeka pia.

Licha ya serikali kudai kutoa misaada ya pesa kwa walioathirika pakubwa na janga la Covid – 19, suala la kodi ya nyumba linazidi kuwa kizungumkuti.

Ili kukwepa gharama zaidi, baadhi ya wakazi Nairobi na viunga vyake, wanahamia nyumba za bei nafuu. “Nilikuwa nikiishi nyumba ya Sh7, 000 kwa mwezi na licha ya kuhamia ya bei nafuu, kodi inakosa,” Nancy Wanjiru, mkazi wa Marurui, Nairobi ameambia Taifa Leo Dijitali kwenye mahojiano.

Sawa na Nancy, Simon Kagombe mkazi na mfanyabiashara Githurai anasema alihama mwezi uliopita baada ya biashara yake ya nguo kuathirika pakubwa. “Mapato yamekuwa ya kula pekee. Inabidi landilodi asubiri kulipwa kodi polepole,” Kagombe akasema, akipongeza mmiliki wa nyumba aliyohamia kwa kujawa na utu.

Ni malandilodi wachache mno wanaoelewa hali wanayopitia wapangaji wakati huu athari za Covid – 19 zinadi kuongezeka. Taswira ya watu kuhama imekuwa ratiba kila wiki, mitaa mbalimbali Nairobi.

Akihojiwa na vituo vya redio vinavyopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili Aprili 2020, Rais Uhuru Kenyatta alisema hana mamlaka kuamuru wamiliki wa nyumba za kupangisha kupunguza kodi au hata kuifuta kwa muda.

Badala yake, Rais aliwahimiza kuwa na ‘utu wakati huu janga hili linatesa ulimwengu’.

You can share this post!

Covid-19: Watu wengi zaidi wapona

Duale apuuza jaribio la kumng’oa afisini

adminleo