MakalaSiasa

KINAYA: ‘Wiper’ ajue ufalme si moto wa sigara kupeanwa, siasa ni weledi wa kamari

April 29th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na DOUGLAS MUTUA

WAKAMBODIA bado wana hasira! Tena nyingi tu. Za nini lakini? Sina hakika, ila juzi wengi wamenitimua kutoka vikundi vyao vya mitandao nilipowatania kuhusu uchaguzi wa urais wa 2022.

Kosa langu ni picha ya kubuniwa kwa tarakilishi iliyomwonyesha Mzee Jomo na mwanawe ‘Kamwana’; Mzee Kirungu na Mwanawe ‘Giddy’ na Mzee Jaramogi na mwanawe ‘Tinga’.

Pia ilimwonyesha ‘Husler’ peke yake, yaani bila baba wala mama, tena kando yake alama ya kumwidhinisha kuwa rais mnamo 2022.

Picha nyingine zote nilizokutajia zilipigwa mstari mwekundu kwa maana kwamba watu hao hawatakikani!

Maandishi mafupi yalieleza isipokuwa ‘Husler’ Kipchirchir Samoei, wengine wote wanatoka jamii za ‘kifalme’ na hivyo basi hawapaswi kuota wakilala Ikulu kuanzia 2022.

Kilichowaudhi Wakambodia zaidi ni kwamba mimi, ‘mtoto wao’, niliwapelekea picha ile isiyokuwa na ‘mtoto wao’ Wiper, kana kwamba sijui ndoto yake ya kulala ikulu ingalipo.

Niliangua kicheko kwa maana napenda matani ya mitandaoni, hata kunihusu, mradi ukweli wa Mungu naujua lakini lo! Kumbe watu bado wananuna na kuomboleza?

Nilipowahoji wawili watatu ambao walijniandikia jumbe kusherehekea ‘kutolewa’ kwangu kikundini, walisema dunia tayari ishawasaliti, hawataki kusalitiwa na watu wao.

Wanahisi kwamba Ikulu inaendelea kusonga mbali nao, miaka ya ‘kijana’ wao nayo inasonga, hakuna matumaini kote jangwani.

Walilalamika kwamba hakuna anayeutambua uwezekano wa Wiper kuongoza Kenya baada ya 2022 ilhali amehadaiwa angeiongoza kuanzia enzi za Mzee Kirungu.

Kumbuka kama fisi alinyemelea mkono wa ‘Baba Jimmy’ ulioning’inia uanguke ili autafune, mzee wa watu akamaliza kipindi chake na kujistaafia kimyakimya.

Bila shaka unajua ‘Wiper’ alichezwa shere na ‘Baba’ alipomuunga mkono kwa fujo mnamo 2013 na mwaka jana kwa ahadi ‘angerudisha mkono’ ikifika 2022.

Wewe nami tunajua kila dalili inaonyesha Wiper atakauka na atoke bila wakati huo ikiwa anatarajia kusaidiwa na ‘Baba’.

 

‘Hasla’ na Kibwana

Niliangua kicheko kingine kikuu kuhusu usaliti nilipomwona kaimu mwenyekiti wa Wiper, mchakataji mkuu wa maembe kutoa juisi, Profesa Kivutha Kibwana, akiwa na ‘Hasla’.

Kumbuka ni huyo huyo ‘Hasla’ ambaye picha yake ilisababisha nifukuzwe vikundi kadha vya mitandaoni nikidhaniwa kumfanyia kampeni.

Unadhani Wakambodia walihisi vipi walipomwona mwenyekiti wao akimzuru ‘Hasla’? Nasikia wengi wamekereka hivi kwamba hata mate hayamezeki.

Wanadhani kuna mambo ya faragha yaliyozungumziwa kati ya Gavana huyo wa Makueni na ‘Husler’, na kuna uwezekano hoja kuu ni kumnyima Wiper Ikulu.

Hasira na pupa za Wakambodia kutaka kumpa Wiper urais zinatokana na hofu kwamba, tukizingatia idadi ya watu, ataiona Ikulu paa.

Huku viongozi wengine wakitafuta miungano ya kieneo ili kupata ushindi, Wiper anaaminika kucheza ligi ndogo ya Tseikuru: kuwachimba Kibwana na ‘Mama Mwenge.’

Siasa ni mchezo wa weledi wa kamari, washindi ni wajanja pekee, si watulivu wanaokalia miguu kusubiri hisani ya watu au kutimizwa kwa ahadi za mdomo tu.

Kamwambie Wiper asipojipanga atapangwa; asipoamini mwambie ‘Husler’ ashabadili sura ya uongozi mlimani, kufanya hivyo jangwani ni mzaha.

‘Ufalme’ si moto wa sigara eti apewe hivihivi tu. Asiseme sikumtahadharisha.

 [email protected]