• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
Madereva wa masafa marefu wahangaika wakisubiri kupimwa Covid-19

Madereva wa masafa marefu wahangaika wakisubiri kupimwa Covid-19

Na WINNIE ATIENO

ZAIDI ya madereva 300 wa masafa marefu waliandamana nje ya Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) wakilalamikia kucheleweshwa kupimwa virusi vya corona.

Madereva hao kutoka humu nchini, na wale wa Uganda, Sudan Kusini, DRC na Rwanda walisema wameachwa kwenye mataa kwa wiki moja sasa baada ya wahudumu wa afya kuwaambia hawawezi kuwapima kwa sababu ya ukosefu wa vifaa maalum vya kutekeleza shughuli hiyo.

Upimaji wa virusi vya corona katika kituo hicho ulisitishwa zaidi ya siku tano zilizopita kufuatia ukosefu wa vipimio.

Maandamano hayo yalijiri siku moja tu baada ya Wizara ya Afya kutangaza kuwa inapitia changamoto za ukosefu wa vifaa vya kupimia.

“Tuna changamoto za vifaa vya kupima virusi vya corona na ndiyo maana kuna hali ya kucheleweshwa,” alisema waziri msaidizi Dkt Rashid Aman.

Hata hivyo, walalamishi hao kupitia muungano wa madereva walisema serikali ina mpango wa kusafirisha mizigo kutoka bandarini kwa kutumia reli ya kisasa – SGR – na kwamba inatishia kuwanyima biashara na ajira.

“Wahudumu wa afya walituambia hawana vifaa vya kupima na tunashinda hapa kila kuchao bila usaidizi. Pia serikali inafaa kutueleza bayana kama ni swala la SGR ndilo linasababisha hali hii,” alisema mkurugenzi mkuu wa muungano huo Bw Dennis Ombok.

Bw David Mwangi, dereva ambaye amekuwa akibeba mizigo kutoka Mombasa, Uganda na hata Sudan Kusini aliisihi serikali kuwaruhusu kusafirisha mizigo kwa kutumia vyeti vya hali yao kiafya kuhusu Covid-19 vilivyopitwa na wakati.

“Nilipimwa mnamo Mei 15 na sikupatikana na virusi lakini cheti changu kimepitwa na wakati. Kwa nini nisiruhusiwe kusafirisha mizigo na kibali changu cha awali? Kwa sasa kuna changamoto ya upimaji,” alisema.

Madereva hao pia walilalamika wakisema wanapitia madhila nchini Uganda huku raia wao wakiendelea kuwanyanyapaa.

“Usalama wetu uko hatarini tukienda Uganda ambako tunakejeliwa na kuitwa corona. Kwa sasa tumekatazwa kuingia bandarini sababu hatujapimwa. Je, tajiri akikataa kutulipa tutaishi vipi?” aliuliza dereva mwingine, Bw Abbass Mwandango.

Naye Bw Anderson Mwandembo alisema anasafirisha vyakula vya msaada kutoka Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kutoka bandarini Mombasa hadi Sudan Kusini.

Dereva kutoka Uganda, Bw Idrisa Yahya alisema alikatazwa kuingia bandarini sababu hajapimwa tangu alipowasili nchini.

“Niliambiwa niende nipimwe tena nikakuja kwenye kituo hiki lakini hakuna vifaa. Tuko zaidi ya madereva 100 kutoka Uganda, Rwanda na DRC hapa Mombasa tukiendelea kuhangaika,” alisema Bw Yahya.?

You can share this post!

Juhudi za kukuza soka ya wanawake zitazaa matunda –...

Karua adokeza kuungana na Mudavadi kuingia Ikulu 2022

adminleo