• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 1:05 PM
Wakulima wa mtama wapinga ada mpya

Wakulima wa mtama wapinga ada mpya

NA GITONGA MARETE

MAELFU ya wakulima katika kaunti za Tharaka Nithi na Meru wamepinga vikali mpango wa kutoza ada mpya ya ushuru kwa mazao ya mtama, wimbi na mihogo wakisema hatua hiyo itawapunguzia mapato.

Wakulima hao hutegemea zao la mtama ambapo wamepewa kandarasi na kampuni ya kutengeneza pombe ya Kenya Breweries Limited aina ya Senator Keg, inayopendwa na wateja wa kipato cha chini.

Hazina Kuu imependekeza kukata ushuru kwa mauzo ya mazo hayo matatu katika kanuni iliyochapisha hivi majuzi na kuwataka wakulima kutoa maoni yao.

Kulingana na KBL, kanuni hiyo mpya inamaanisha bei ya pombe hiyo itapanda kwa Sh10 kwa kila mililita 300 hali ambayo inatarajiwa kupunguza wateja na hivyo kupunguza kiwango cha mtama inachonunua kwa wakulima hao.

Katika kaunti hizo mbili, kuna zaidi ya wakulima 30,000 walio kwa mkataba wa kukuza mtama kwa niaba ya KBL ambapo inanunua kila kilo kwa Sh32, na kuwapa wakulima soko tayari za zao hilo.

Beatrice Nkatha, mratibu wa muungano wa wakulima hao, alisema kuwa serikali inafaa kujali maslahi ya wakulima hao wasio na mbonu nyingine ya kupata riziki, na kusitisha mpango wa kuwakata ada kwa mauzo.

“Hatuelewi sababu ya serikali kutaka kuzamisha mmea ambao unategemewa na watu wasiojiweza kiuchumi. Tumetuma mapendekezo yetu kwa serikali tukiomba ibatilishe mpango huo,” alisema Bi Nkatha.

You can share this post!

Nyanya na vitunguu ghali zaidi, viazi na karoti zashuka bei

Deni la Kenya sasa lafika Sh6.28 trilioni

adminleo