Habari Mseto

Kafyu kuanza saa tatu usiku

June 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA SAMMY WAWERU

Muda wa kafyu ya kitaifa inayoendelea kutekelezwa kila siku umeongezwa kwa siku 30 zaidi.

Kufuatia mkurupuko wa ugonjwa wa Covid – 19 nchini, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuanza kutekelezwa kwa amri ya kutotoka nje kati ya saa moja za jioni hadi saa kumi na moja za asubuhi kuanzia Machi 27, 2020 ili kudhibiti maambukizi zaidi.

Mnamo Jumamosi, Wakenya walikuwa na matumaini makuu kwamba masharti yaliyowekwa yangelegezwa na amri hiyo kuondolewa, lakini katika hotuba ya Rais Kenyatta alitangaza kuongezwa kwa muda zaidi.

“Baada ya kutathmini na kusikiliza maelezo ya wataalamu na watafiti, ikizingatiwa kuwa maambukizi yanaendelea kuongezeka, tumeafikia kuongeza muda wa kafyu kwa kipindi cha siku 30 zaidi,” Rais akatangaza, kwenye hotuba yake kwa taifa katika Ikulu, Nairobi.

Rais amesema uamuzi huo umetokana na tathmini ya athari zinazoweza kutokea endapo kafyu inayoendelea itaondolewa. Tangu kafyu ianze kutekelezwa, kiongozi wa nchi amesema amri hiyo imezuia maambukizi zaidi kushuhudiwa.

Hata hivyo, saa za amri hiyo kutekelezwa zimetathminiwa, saa za kuanza zikisongeshwa hadi saa tatu usiku na kukamilika saa kumi asubuhi.

Rais Kenyatta amesema mabadiliko hayo yatawezesha Wakenya kurejelea katika ratiba ya kawaida ya utendakazi, akieleza kwamba hatua hiyo itasaidia kufufua uchumi.

“Mabadiliko hayo yatasaidia Wakenya kuwa na ratiba kamilifu ya kila siku kufanya kazi,” akasema.

Akitetea kuendelea kutekelezwa kwa kafyu ya kitaifa, Rais Kenyatta alisema wataalamu na watafiti wameonya kwamba kuiondoa ni kuhatarisha maisha ya Wakenya.