Mahangaiko ya mafuriko shule zikifunguliwa
Na WAANDISHI WETU
MAFURIKO na maporomoko ya ardhi yanayoendelea kushuhudiwa katika pembe nyingi za nchi yamesababisha mahangaiko makubwa. Mbali na vifo, kuna baadhhi ya kaunti ambazo zimefunikwa kabisa na maji ya mvua.
Katika kaunti ya Tana River, Gavana Dhadho Godhana alisema Jumapili kuwa asilimia 70 ya wakazi wameathiriwa huku watu 11 wakifa kwa kusombwa na mafuriko.
Akihutubia wanahabari jijini Nairobi, Gavana Dhadho alisema miongoni mwa waliokufa ni watoto walio na umri wa chini ya miaka kumi akiwemo mmoja wa miezi minane.
Mkasa huu umeathiri asilimia 70 ya wakazi. Tumepoteza watu 11,” alisema.
Gavana huyo alisema mbali na mto Tana kuvunja kingo zake, mito mingine midogo inayoanzia kaunti za Kitui na Makueni imejaa maji na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na watu kupoteza maisha.
“Katika baadhi ya maeneo watu wanaishi katika kambi 106. Familia 38,000 zimeathiriwa moja kwa moja na mafuriko,” aliongeza Gavana Dhadho.
Alisema kwa jumula watu 228,000 wameathiriwa na wanakabiliwa na hatari ya kupata maradhi, hawana makao, chakula, dawa, maji safi na mahitaji mengine.
“Watu wanaoishi kando ya mto Tana wanakabiliwa na tisho kuu la njaa baada mimea yao kuharibiwa na mafuriko,” alisema.
Hali ya uchukuzi pia imeathiriwa na misaada inaweza kupelekwa kwa ndege au kwa mashua.
Gavana Dhadho alitoa wito kwa mashirika ya kutoa misaada kujitokeza kuungana na serikali yake kusaidia waathiriwa. Kamishna wa kaunti hiyo Michael Kioni alisema Kaunti ndogo ya Tana Kaskazini ndiyo imeathirika sana ambapo familia 16,000 zimeathirika ikifuatiwa na ile ya Tana Delta ambapo familia 14,000 zimeathirika. Kaunti ndogo ya Tana River ni ya tatu ambayo ina waathiriwa 8,000.
Wakati huo huo watu wanane walikufa baada ya kusombwa na mafuriko katika visa tofauti Kaunti ya Kisii kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha kote nchini.
Katika kisa cha kwanza mwanamume alisombwa na maji katika eneo la Nyambunde, Kaunti ndogo ya Bobasi alipokuwa akivuka daraja kwenye mto Gucha uliofurika.
Katika kisa cha pili eneo la Ogembo wanaume wawili walipoteza maisha yao baada ya kusombwa na maji walipokuwa wakijaribu kuvuka mto huo.
Mvua hiyo ilisababisha uharibifu mkubwa kwenye mashamba ya watu huku nyua za nyumba za makazi karibu na mto huo zikiharibiwa pia.
Eneo la Daraja Mbili, mjini Kisii mwanaume wa umri wa miaka 40, alikufa maji baada ya kujaribu kuvuka daraja na kusombwa na mto Nyakomisaro.Watu zaidi ya 100 kutoka maeneo ya Mugirango Kusini na Bobasi, hawana makazi baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko.
Akithibitisha visa hivyo msimamizi wa idara ya majanga katika Kaunti ya Kisii Dkt Walter Okib alisema kuwa mvua hiyo imesababisha hasara kubwa katika maeneo yaliyo kando na kuchukuwa maisha ya watu.
Mtu mmoja alikufa na zaidi ya familia 2,000 zikaathiriwa Mandera Kusini. Mji wa Elwak ndio ulioathiriwa zaidi.
Ripoti za BENSON MATHEKA, JADSON GICHANA, MANASE OTSIALO, BRIAN OCHARO na STEPHEN ODUOR