• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Jopo la BBI laelekea Mombasa kumalizia ripoti

Jopo la BBI laelekea Mombasa kumalizia ripoti

Na WALTER MENYA

JOPO la Mpango wa Maridhiano (BBI) litaelekea jijini Mombasa kwa kikao maalum kuanzia kesho, kwenye harakati za mwisho mwisho za kuandaa ripoti yake.Muda wa jopo hilo unatarajiwa kumalizika rasmi hapo Juni 30.

Na linapojitayarisha kwa hatua za mwisho, imeibuka kuwa masuala makuu yaliyogusiwa pakubwa ni ujumuishaji wa jamii zaidi kwenye mfumo wa utawala wa nchi, vita dhidi ya ufisadi, umoja, ustawi wa nchi na ugatuzi.

Jopo hilo limekuwa likifanya kazi katika makundi mbalimbali, ili kuangazia mapendekezo ya kikatiba na kisheria yaliyowasilishwa kwake na Wakenya.

Duru ziliiambia Taifa Jumapili kwamba shughuli kuu kwenye kikao hicho itakuwa ni uandishi na tathmini wa kina kuihusu.

“Tumepiga hatua kubwa. Tutakuwa tumemaliza kila kitu katika muda wa wiki mbili zijazo,” zikaeleza duru.

Kikao hicho kitafanyika katika eneo la siri, ili kuepuka usumbufu wowote.Kikao kitawaleta wanachama wote wa Kamati Kuu na wataalamu 30 walioteuliwa, baada ya uzinduzi wa ripoti hiyo mnamo Novemba katika Ukumbi wa Bomas mnamo Novemba.

Wataalamu hao watalisaidia jopo kushughulikia na kulainisha mapendekezo makuu kwenye ripoti. Baada ya kikao hicho, jopo hilo litatathmini upya ripoti hiyo, ambapo baadaye litaikabidhi kwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Kamati Kuu inaongozwa na Seneta Yusuf Haji wa Garissa kama mwenyekiti. Makatibu wake ni Bw Martin Kimani na wakili Paul Mwangi.

Wataalamu hao waliteuliwa kufuatia pendekezo la kamati kuhusu hitaji la kujumuishwa kwao, ili kuisaidia kuiboresha ripoti na kuimaliza katika muda iliyopewa.

You can share this post!

JAMVI: Uhuru akanganya wanasiasa kwa karata wasioelewa

Hatujaathiriwa na corona – Ulinzi Stars

adminleo