• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
SAKA ASAKWA: Liverpool wajitosa katika vita vya kuwania huduma za chipukizi matata

SAKA ASAKWA: Liverpool wajitosa katika vita vya kuwania huduma za chipukizi matata

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

LIVERPOOL wamejitosa katika vita vya kuwania huduma za chipukizi matata wa Arsenal, Bukayo Saka ambaye sasa ametaka Arsenal kusitisha mazungumzo kuhusu uwezekano wa kurefusha mkataba wake uwanjani Emirates.

Saka, 18, amekuwa kivutio kwa vikosi vingi vya bara Ulaya tangu apate nafasi ya kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Arsenal baada ya mabeki Sead Kolasinac na Kieran Tierney kujeruhiwa.

Japo ni matamanio ya kocha Mikel Arteta kuendelea kujivunia maarifa ya Saka kwa miaka mitano zaidi, huenda kinda huyo akashawishika kuyoyomea Liverpool baada ya wakala wake kufichua kwamba anatawaliwa na kiu ya kusakata soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Kufikia sasa, Saka anajivunia kuchangia mabao tisa kutokana na mechi 29 zilizopita ndani ya jezi za Arsenal.

Alipangwa katika kikosi cha kwanza cha Arsenal kwa mara ya kwanza mwaka jana katika kivumbi cha Europa League chini ya kocha Unai Emery aliyetimuliwa Novemba 2019.

Mbali na Liverpool, klabu nyingine inayokeshea maarifa ya Saka ni Borussia Dortmund ya Ujerumani ambayo imepania kumsajili iwapo itaagana na Jadon Sancho anayehusishwa na uwezekano mkubwa wa kujiunga na Manchester United kwa kima cha Sh17 bilioni.

Akijivunia jumla ya mabao 17 na kuchangia mengine 19 hadi kufikia sasa muhula whuu, Sancho, 20, anawaniwa pia na Juventus, Real Madrid na Bayern Munich.

Gazeti la The Sun limesisitiza kwamba Saka atakuwa radhi kupokea mamilioni ya Dortmund au Liverpool badala ya Sh420,000 pekee ambazo kwa sasa analipwa kwa wiki uwanjani Emirates.

Kinda huyo angali na mwaka mmoja pekee katika kandarasi yake na Arsenal ambao wameanza kumvizia chipukizi Jude Bellingham, 16, wa Birmingham katika juhudi za kuziba pengo litakaloachwa na Saka.

Wakati uo huo, Liverpool wamemweleza Philippe Coutinho kwamba hawapo tayari kuwania upya huduma zake mwishoni mwa msimu huu baada ya ajenti wa kiungo huyo, Kia Joorabchian, kuulizia uwezekano wa kurejea kwa mteja wake ugani Anfield.

Coutinho ametatizika sana kufufua makali aliyokuwa akijivunia zamani uwanjani Anfield kabla ya kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Barcelona mnamo Januari 2018.

Barcelona walimshawishi Coutinho, 27, kuagana na Liverpool kwa kima cha Sh14 bilioni japo akashindwa kusadikisha mashabiki wa miamba hao kwamba alistahili kununuliwa kwa kiwango hicho cha fedha.

Kushindwa kwake kutamba ugani Camp Nou ni kiini cha Barcelona kumtuma kwa mkopo wa mwaka mmoja kambini mwa Bayern Munich mwanzoni mwa msimu huu.

Japo ilitarajiwa kwamba Bayern wangalikuwa wepesi wa kumpokeza mkataba wa kudumu, mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) hawajaonyesha ari ya kuziwania huduma za nyota huyo mzawa wa Brazil.

Badala yake, ameanza kuhusishwa na uwezekano mkubwa wa kuingia kambini mwa Leicester City ambao kwa sasa watalazimika kuwapiga kumbo Everton, Chelsea na Man-United.

You can share this post!

Corona imeisha Tanzania – Magufuli

Eastleigh yaamka tena kibiashara baada ya majuma kadhaa ya...

adminleo