Gavana Mvurya aamuru masoko yafunguliwe Kwale japo kwa masharti
Na WINNIE ATIENO
GAVANA Salim Mvurya ameanza kufungua uchumi wa Kwale baada ya kuidhinisha kufunguliwa kwa masoko katika kaunti hiyo.
Hii ni afueni kwa wafanyabiashara ambao walikuwa wanalalamika baada ya biashara sokoni kusitishwa ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.
Hata hivyo, wafanyibiashara na wachuuzi watatakiwa kufuata maagizo ya Wizara ya Afya ikiwemo kuosha mikono kwa kutumia maji na sabuni, kuvaa barakoa na kudumisha umbali wa mita moja na zaidi baina ya watu na pia kuepuka safari zisizokuwa za lazima.
Bw Mvurya amesema hatua ya kufungua masoko inalenga kufufua uchumi wa kaunti ya Kwale ambao ulidororoa kufuatia janga la Covid-19.
Amewataka wahudumu wa bodaboda na tuktuk kuendelea kubeba abiria waliojikinga dhidi ya virusi hivyo kwa kuvaa barakoa.
“Hamruhusiwi kubeba abiria idadi zaidi ya iliyopendekezwa. Masoko yetu ya wazi na yale ya mifugo ambayo yalifungwa kufuatia janga hili yataanza kuhudumu, lakini tunawasihi wakazi, wachuuzi na wafanyabiashara wote wa hapa waweke mikakati ya kuhakikisha wanajikinga dhidi ya virusi vya corona,” amesema baada ya kikao na kamati ya dharura ya kupambana na maradhi hayo.
Kadhalika, yeyote anayedhamiria kusafiri kaunti hiyo ama kutoka Mombasa au nchini Tanzania anatakiwa kuwa na cheti cha kutathmini dhamira yake na “wote watapimwa ili kuhakikisha hawana virusi vya corona.”
Gavana amesema maafisa wa usalama na wahudumu wa afya wataendelea kushika doria kwenye mikapa hiyo kuhakikisha watu wenye virusi hawatorokei katika kaunti hiyo.
“Kama unakuja Kwale kutoka sehemu nyingine lazima uwe na sakabadhi maalum kuelezea dhamira na pia tutakupima kuhakikisha huna virusi. Tunafanya hivi ili kulinda afya za wakazi wa Kwale,” ameongeza.