Michezo

Simbas kutumia kipute cha raga ya Afrika kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia

June 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KIPUTE cha kuwania Raga ya Kombe la Afrika mnamo 2022 sasa kitatumiwa na Kenya Simbas kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mnamo 2023 nchini Ufaransa.

Kivumbi cha Africa Cup hakijafanyika kwa kipindi cha misimu miwili iliyopita kutokana na uchechefu wa fedha na janga la corona mtawalia. Kampeni hizo zitarejelewa mwakani.

Mshindi wa Africa Cup atajikatia tiketi ya moja kwa moja ya kuingia fainali za Kombe la Dunia huku nambari mbili akilazimika kushiriki mchujo dhidi ya vikosi vingine vitatu kutoka mashirikisho tofauti.

Timu 12 tayari zimefuzu kwa fainali za 2023 nchini Ufaransa baada ya kukamata nafasi tatu za kwanza kwenye kampeni zao za Raga ya Dunia (RWC) katika msimu wa 2019. Hizi ni pamoja na Afrika, Uingereza, New Zealand, Wales, Japan, wenyeji Ufaransa, Australia, Ireland, Scotland, Italia, Argentina na Fiji.

Nafasi nane zilizosalia zitaamuliwa kupitia mchakato wa timu kushiriki mapambano ya mchujo katika kiwango cha kimaeneo. Shughuli hiyo itakamilika kwa mchujo wa mwisho utakaoshirikisha timu nne za mwisho mnamo Novemba 2022. Tarehe za kuandaliwa kwa mashindano ya msimu wa 2021 zitatolewa mapema wiki ijayo.

Kenya Simbas walikosa tiketi ya kunogesha fainali za Kombe la Dunia mnamo 2019 baada ya kuzidiwa maarifa na Canada kwenye mchujo wa mwisho uliotawaliwa na Ujerumani na Hong Kong nchini Ufaransa.

Chini ya kocha Paul Odera, Kenya Simbas watakuwa wakiwania fursa ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia.

Mnamo 2018, Simbas waliambulia nafasi ya pili barani Afrika baada ya kuwapepeta Uganda, Tunisia na Zimbabwe kabla ya chombo chao kuzamishwa na Namibia jijini Windhoek.

Mnamo 2015, walikosa padogo kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Uingereza baada ya Zimbabwe kuwazaba 27-10.

Awali, Kenya ilikuwa imewapiga wenyeji Madagascar 34-0 na Namibia ambao hatimaye waliwakilisha bara la Afrika kwa 29-22 katika hatua ya makundi.

Odera amesema kutoandaliwa kwa Kombe la Afrika katika kipindi cha miaka miwili mfululizo ni pigo kubwa kwa maandalizi ya kikosi chake ambacho sasa hakitashiriki mapambano yoyote ya haiba kubwa mwaka huu.

“Yasikitisha kwamba tutakuwa na mwaka mmoja pekee wa kujiandaa kwa mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia. Ingawa jambo hili linatuweka katika hali ngumu, naamini ukubwa wa uwezo wa vijana wangu” akasema.

Mechi za Simbas katika Kombe la Afrika zilitarajiwa kuanza dhidi ya Morocco kisha Ivory Coast, Uganda na Zimbabwe.