Habari

Wandani wa Ruto eneo la Rift Valley sasa wafyata ndimi

June 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

ERIC MATARA na CHARLES WASONGA

BAADHI ya wabunge na maseneta kutoka Rift Valley ambao wamekuwa watetezi sugu wa Naibu Rais William Ruto wameingiwa baridi baada Rais Uhuru Kenyatta kuwaondoa wenzao kutoka nyadhifa za uongozi katika seneti na bunge la kitaifa.

Wengi wao nyakati hizi hawaonekani hadhari wakimpigia debe Dkt Ruto tangu mapema mwezi Mei mjeledi wa Rais ulipowacharaza maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) na Susan Kihika, waliopokonywa nyadhifa za kiongozi wa wengi na kiranja wa wengi, mtawalia.

Seneta wa Tharaka-Nithi Kithure Kindi pia alivuliwa wadhifa wa Naibu Spika, cheo ambacho sasa kinashikiliwa wa Seneta wa Uasin Gishu Profesa Margaret Kamar.

Mwandani wa Ruto wa hivi punde kubadili msimamo na kutangaza uaminifu wake kwa Rais Kenyatta ni Mbunge Maalum David Sankok na Seneta Maalum Victor Prengei.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bw Sankok alisema kando na kukariri uminifu wake kwa Kiongozi huyo wa Jubilee, vilevile anaunga mkono mchakato wake wa kuzima uasi ndani ya chama hicho.

“Namuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta katika yale anayofanya kusafisha chama chetu. Ni kiongozi wangu wa chama na bosi wetu; tunamheshimu. Akiitisha mkutano wa wabunge, sharti tuhudhurie na kutoa maoni yetu. Kwa hakika wale ambao hawamuungi mkono rais na manifesto ya Jubilee, ilhali walichaguliwa kwa tiketi ya chama hiki, wanapaswa kujiuzulu na washiriki uchaguzi mdogo,” akasema Bw Sankok ambaye anawakilisha watu wanaoishi na ulemavu.

Mbunge huyo alimpongeza Rais Kenyatta kwa kubuni ushirikiano na vyama vingine kwa nia ya kufanikisha ahadi alizotoa kwa Wakenya.

Seneta Prengei, ambaye ni miongoni mwa maseneta watano wanaokabiliwa na tishio la kufurushwa kutoka Jubilee kwa kususia mkutano wa maseneta katika Ikulu ya Nairobi mwezi jana, pia amebadili msimamo na kujiunga na mrengo unaomuunga mkono Rais Kenyatta.

Mmoja wa wandani wake alisema hivi: “Anaunga mkoni Rais Uhuru Kenyatta. Ama kwa hakika ni mmoja wa maseneta walipiga kura kuunga mkono hoja ya kumng’oa mamlakani Profesa Kindiki.”

Na katika kaunti ya Nakuru ambako Dkt Ruto amekuwa akiungwa mkoni na wabunge wengi. Wengi wa wabunge hao ambao wamekuwa wakimtetea Dkt Ruto kwa vinywa vipana, sasa wamekimya na kuingiwa baridi; hawaonekani tena hadharani.

Baadhi yao wanasema wameamua kutumia wakati wao mwingi katika kile wanachotaja kama “shughuli za maendeleo katika maeneo bunge yao.”

Mbunge wa Nakuru Mjini Magharibi Samuel Arama ambaye ni Mbunge wa kipekee katika eneo hilo ambaye amekuwa akimuunga mkono Rais Kenyatta hadharani, alifichua kuwa baadhi ya wandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakimfikia wakitaka kujiunga na kambi ya Rais Kenyatta

“Tuko tayari kufanyakazi na mtu yeyote ambaye anaunga mkono ajenda ya serikali. Chama cha Jubilee kina manifesto ambayo Rais anataka kutekeleza. Na kwa kufanya hivyo anahitaji uungwaji mkono na heshima kutoka kuwa wanachama wa Jubilee,” akasema Bw Arama.

Kaunti ya Nakuru ambayo ni ngome ya Jubilee ina jumla ya wabunge 11 na wote na wandani wa Naibu Rais Dkt Ruto, isipokuwa Bw Arama.

Wandani wa Ruto katika kaunti hiyo wanajumuisha Seneta Kihika na wabunge, Kimani Ngunjiri (Bahati), David Gikaria (Nakuru Mjini Mashariki), Samuel Gachobe (Subukia), Jayne Kihara (Naivasha) na Martha Wangari (Gilgil).

Wengine ni Joseph Tonui (Kuresoi Kusini), Moses Cheboi (Kuresoi Kaskazini), Kuria Kimani (Molo), Charity Kathambi Chepkwony (Njoro) na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti Lisa Chelule.

Viongozi hawa wamenyamaza kwa hofu kuwa Rais akaelekeza vita katika maeneo bunge yao na kupelekea wao kupoteza uchaguzi mkuu wa 2022.

Juzi Bw Ngunjiri, Bw Gikaria, Seneta Kihika, na wengine walijitokeza wazi na kusema kuwa wako tayari kuunga mkono mpango wa maridhiano (BBI) unaendesha na Rais Kenyatta pamoja na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Hata hivyo, ni Mheshimwa Tonui pekee ndiye ameshikilia kuwa ataendelea kurindima wimbo wa Dkt Ruto