• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
Thiago Silva awaniwa na klabu tano za EPL

Thiago Silva awaniwa na klabu tano za EPL

Na MASHIRIKA

THIAGO Silva amesema atahiari kusalia katika mojawapo ya klabu za bara Ulaya kwa misimu miwili zaidi baada ya waajiri wake Paris Saint-Germain (PSG) kumweleza kwamba hawatarefusha mkataba wake mwishoni mwa muhula huu.

Ingawa anawaniwa pakubwa na klabu maarufu nchini Amerika na China, beki huyo mzawa wa Brazil mwenye umri wa miaka 35 angali na matamanio ya kusakata soka ya ushindani mkubwa zaidi baada ya vikosi vitano vya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kuanza kumnyemelea.

Mbali na Arsenal ambao wanapania kumfanya awe kizibo cha David Luiz, klabu nyingine zinazomhemea Silva ni Newcastle United, West Ham United, Everton na Wolves.

Kiini cha Silva kutaka kusalia barani Ulaya hata iwapo atapunguziwa mshahara kutoka Sh30 milioni anazopokea kwa sasa mwishoni mwa kila wiki, ni maazimio ya kupangwa katika timu ya taifa ya Brazil wakati wa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Silva anataka kustaafu rasmi kwenye ulingo wa soka mwishoni mwa fainali hizo.

Silva amekuwa nahodha na beki tegemeo la PSG katika kipindi cha misimu minane iliyopita.

Kocha wa Napoli, Gennaro Gattuso aliyewahi kucheza pamoja na Silva kambini mwa AC Milan, pia yuko radhi kumsajili Mbrazil huyo iwapo Milan wataagana na beki Kalidou Koulibaly anayehusishwa na uwezekano wa kutua Manchester United.

Ingawa hivyo, amefichua azma ya kutaka kuungana na kocha wake za zamani wa Milan, Carlo Ancelotti ambaye kwa sasa anadhibiti mikoba ya Everton.

Silva aliondoka Milan kwa pamoja na Zlatan Ibrahimovic mnamo 2012 na familia yake imemtaka sana arudi Italia ndipo astaafu akinogesha kivumbi cha Serie A sawa na alivyofanya mfumaji mkongwe Ibrahimovic.

Mbali na waajiri wake wa zamani nchini Brazil, Fluminense kumvizia, huduma za Silva zinamezewa mate vilevile nchini Japan na Qatar wanaotaka abadilishe uraia.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali isilemaze Wakenya kwa kodi

Wetang’ula angali kiongozi wa Ford-Kenya

adminleo