• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Ndayishimiye kuapishwa awe Rais wa Burundi haraka iwezekanavyo

Ndayishimiye kuapishwa awe Rais wa Burundi haraka iwezekanavyo

MASHIRIKA na CHARLES WASONGA

GITEGA, BURUNDI

MAHAKAMA ya kikatiba ya Burundi imeamua kwamba Rais mteule Evariste Ndayishimiye ndiye anapawa kuapishwa mara moja baada ya kifo cha Pierre Nkurunziza, serikali imesema Ijumaa.

Majaji wa mahakama hiyo walitoa uamuzi huo licha ya Katiba ya nchi kupendekeza kuwa Spika wa Bunge la Kitaifa ndiye anapaswa kuingia mamlakani, kwa muda, baada ya kifo cha Rais.

Hata hivyo, mahakama hiyo imeamua kwamba hamna haja ya kuwepo kaimu Rais kwani Ndayishimiye tayari alikwisha kutangazwa mshindi katika uchaguzi wa urais uliofanyika mwishoni mwa mwezi Mei.

“Mahakama imekatalia mbali wazo la kuwa na Rais atakayeshikilia kwa muda,” serikali ilisema kwenye taarifa iliyochapisha katika mtandao wa Twitter.

Baada ya Rais Nkurunziza kufariki Jumanne, maafisa wa serikali wamekuwa wakijadiliana kuhusu ni nani anapaswa kuingia mamlakani.

Hali hiyo iliibua wasiwasi kwamba huenda majenerali wa kijeshi wangeanza kung’ang’ania mamlaka na hivyo kutumbukiza nchi hiyo katika vita.

Hata hivyo, taarifa ya Ijumaa haijabainisha ni lini hafla ya kuapishwa kwa Ndayishimiye itafanyika.

Ndayishimiye ambaye alidhaminiwa na chama tawala cha CNDD/FDD alitangazwa mshindi katika uchaguzi wa urais wa Mei baada ya kumbwaga mgombea wa upinzani Agathon Rwasa.

Alikuwa ameratibiwa kuapishwa mnamo Agosti 2020 na kuchukua hatamu za uongozi rasmi kutoka kwa Nkurunziza.

Huu ndio ulikuwa uchaguzi wa kwanza, wenye ushindani, nchini Burundi tangu kutokee vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo 1993.

Marehemu Nkurunziza ni kiongozi wa zamani wa waasi ambaye uongozi wake ulilaumiwa kwa kusheheni vitendo vya ukatili dhidi ya wanasiasa wapinzani wake.

Uongozi kama huu ulichangia uchumi wa Burundi kuzorota baada ya wafadhili kukatiza misaada yao ya kifedha kwa taifa hilo kutokana na ongezeko la visa vya ukiukaji haki.

You can share this post!

Mbappe, Sterling na Sancho waongoza kwa thamani ya...

Wazee wa Kalenjin wazidi kugawanyika kuhusu Ruto

adminleo