Bajeti Kuu yatenga Sh1.7 bilioni kwa barabara za Kiambu
Na LAWRENCE ONGARO
KAUNTI ya Kiambu itanufaika na takribani Sh1.7 bilioni zitakazoelekezwa kwa miradi ya ujenzi wa barabara kutokana na bajeti ya serikali.
Kati ya fedha hizo Sh700 milioni zitatumika Thika na vitongoji vyake kukarabati barabara za eneo hilo.
Mbunge wa Thika alikuwa wa kwanza kuishukuru serikali kwa kuipatia mgao kaunti mzima ya Kiambu huku akisema ni afueni kubwa kwa wananchi kwa jumla.
Kulingana na mbunge huyo, awamu ya kwanza ni mradi wa barabara ya umbali wa kilomita 18 ambayo itakuwa eneo la Gatuanyaga-Munyu hadi Kang’ok. Ni mradi utakaoendeshwa na Halmashauri ya Barabara za Mijini – Kenya Urban Roads Authority – KURA.
Kulingana na mpango wa Halmashauri hiyo, barabara hiyo itaanza katika eneo la Gatuanyaga(A3) ikielekea Munyu hadi Githima na kufika Kang’oki (Dumpsite).
Bw Wainaina alisema tayari upimaji wa barabara hiyo umekamilika ambapo imesalia kazi kuendelea.
“Wakazi wa Githima, Komo, na Gatuanyaga kwa muda mrefu wamekuwa katika hali ngumu kibiashara ambapo mvua ikinyesha biashara nyingi huathirika,” alisema mbunge huyo.
Bajeti hiyo imeleta matumaini kwa wakazi wa Thika kwa jumla na baadhi waliohojiwa wanaksema ya kwamba huo ni kama mwamko mpya kwao.
“Kwa muda mrefu tumekuwa na barabara mbovu ambazo zimetuletea hasara kubwa tukiendesha biashara zetu. Tunaamini kuwa barabara ikikamilika kila mfanyabiashara eneo hili atanufaika,” alisema Francis Maina ambaye ni mwendeshaji bodaboda mjini Thika.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika, Bw Alfred Wanyoike alipongeza juhudi za serikali kufanya kweli na kuona ya kwamba Kaunti ya Kiambu haibaki nyuma katika maendeleo.
“Tayari nimepokea pongezi tele kutoka kwa wafanyabiashara na washikadau wengi walisema hatua ya kujengewa barabara ni mwamko mpya utakaoleta maendeleo kwa kila mkazi,” alisema Bw Wanyoike.
Alisema kwa vile mji wa Thika ni wa viwanda vingi, bila shaka biashara zitanawiri kwa kiwango cha juu huku nafasi za kazi pia zikipatikana.