• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 AM
Mbunge ahimiza viongozi katika ngazi zote waonyeshe uadilifu

Mbunge ahimiza viongozi katika ngazi zote waonyeshe uadilifu

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kila Mkenya kuwa makini kupambana na ugonjwa wa Covid-19 kwa lengo la kupunguza makali yake na kuenea kwake.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina, alisema Ijumaa hata mambo yakirejea kawaida, itakuwa muhimu kwa kila mmoja kuwa makini na mienendo yake.

Akihojiwa na kituo cha upeperushaji mtandaoni cha Club Life – Thika 237 Connect, alisema wananchi wanastahili kuwachagua viongozi wenye maadili mema na uwajibikaji.

“Ili wananchi waweze kupata viongozi wazuri ni vyema kutathmini aina ya viongozi wanaofaa kulinda mali yao,” alisema Bw Wainaina.

Aliwashauri vijana ambao ndio wameshikilia asilimia kubwa ya kura, kuwa mstari wa mbele kutafuta viongozi wenye maadili mema.

“Hakuna haja ya vijana kila mara kulalamika kuhusu uongozi mbaya huku hao wenyewe wakiwa ndio waliowachagua viongozi hao wabaya,” alisema mbunge huyo.

Anataka viongozi kutoka kiwango cha diwani, mbunge, seneta, na hata gavana wawe watu wanaowajibika ili nchi ifikie kiwango cha kutamanika na wengi.

Alitoa mfano wa kzi ya ugavana akisema haitaki viongozi walafi bali inataka yule anayewajibika aliye na ari ya kutumikia wananchi bila mapendeleo.

“Gavana ni kiongozi anayejua sekta zote za eneo lake na kutambua kila kiongozi aliye chini yake anaendesha vipi idara aliyopewa,” alifafanua Bw Wainaina wakati wa mahojiano.

Alipongeza hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kurejesha uongozi wa Kaunti ya Nairobi chini ya serikali kuu.

“Hatua hiyo kulingana naye ilikuwa sawa kwa sababu jiji la Nairobi halifai kuletewa mzaha. Wageni wa kimataifa hufika hapo kwa mikutano mikubwa na kwa hivyo mpangilio wake unastahili kuwa wa hadhi ya juu,” alieleza Bw Wainaina.

Kuhusu mpango wake wa siku zijazo, alisema kwa wakati huu anatumikia wakazi wa Thika kama mbunge, lakini wakitaka kumuinua katika kiwango kingine yeye ni nani akatae?

Aliwashajiisha viongozi popote walipo wawe na ukweli kwa wananchi na watekeleze ahadi zote wanazotoa kwa wapigakura.

You can share this post!

Bajeti Kuu yatenga Sh1.7 bilioni kwa barabara za Kiambu

PWANI: Uwanja wa Tononoka kukarabatiwa uwafae wanasoka

adminleo