Habari Mseto

Wakenya wanataka makanisa yafunguliwe – Ripoti

June 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

IDADI kubwa ya Wakenya wanataka waruhusiwe kwenda kuabudu makanisani na misikitini huku wakipinga mpango wa serikali kutaka shule zifunguliwe kuanzia Septemba, mwaka huu.

Ripoti ya utafiti wa kura ya maoni iliyotolewa jana na Infotrak inaonyesha kuwa asilimia 59 ya Wakenya wanataka serikali iondoe vikwazo vinavyowazuia kwenda kuabudu makanisani na misikiti.

Maeneo ya Pwani na Magharibi ndiyo yanaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wanaotaka waruhusiwe kwenda misikitini na makanisani kuabudu kwa asilimia 77 na 64 mtawalia.

Hata hivyo, idadi kubwa ya wakazi wa Nyanza (asilimia 53) wanataka maeneo ya ibada yaendelee kufungwa.

Idadi kubwa ya wakazi wa mijini (asilimia 65) wanataka maeneo ya ibada yafunguliwe ikilinganishwa na asilimia 57 ya wenzao wa vijijini.

Kulingana na ripoti hiyo, asilimia 70 ya Wakenya wanapinga kufunguliwa kwa shule kutokana na hofu kwamba hatua hiyo huenda ikasababisha kusambaa kwa virusi vya corona miongoni mwa wanafunzi.

“Wanaopinga kufunguliwa kwa shule wanasema kuwa itakuwa vigumu kuzuia wanafunzi kucheza pamoja. Kadhalika, wanasema, ni rahisi kwa wanafunzi kusahau kufuata kanuni zilizowekwa za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona kama vile kutotangamana, kuvalia barakoa na kunawa mikono mara kwa mara,” inasema ripoti ya utafiti huo.

Ukanda wa Nyanza unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wakazi wanaotaka shule ziendelee kufungwa hadi mwaka ujao kama njia mojawapo ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Lakini idadi kubwa ya wakazi wa Kaskazini Mashariki (asilimia 44) na Magharibi (asilimia 37) wanataka shule zifunguliwe kuanzia Septemba wanafunzi waendelee na masomo yao.

Utafiti huo uliofanywa kati ya Mei 2 na Juni 2 miongoni mwa watu 1,200 kutoka kote nchini, unaonyesha kuwa wananchi wanahofia kuwa wanafunzi huenda wakawa kiini cha maambukizi ya virusi vya corona hivyo kuhatarisha maisha ya wazee.

Rais Uhuru Kenyatta katika hotuba yake ya Juni 6, aliagiza wizara ya Elimu kuweka mikakati kuhakikisha kuwa shule zinafunguliwa kwa awamu kuanzia Septemba 1, mwaka huu.

Waziri wa Elimu George Magoha anatarajiwa kutoa mwongozo kuhusu jinsi shule zitafunguliwa bila kuhatarisha maisha ya wanafunzi.

Utafiti huo pia unaonyesha kuwa wazazi wamechukua hatua mbalimbali za kulinda watoto wao dhidi ya kupatwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Kwa mfano asilimia 68 ya wakazi wa Nyanza na Kaskazini Mashariki walisema kuwa wanavalisha watoto wao barakoa wanapotoka nje kwenda kucheza na wenzao. Asilimia 69 ya wakazi wa Mashariki, Pwani (54), Bonde la Ufa (56), Kati (44), Nairobi (52) na Magharibi (52) pia walisema kuwa wanavalisha watoto wao barakoa mara kwa mara.

Idadi kubwa ya wazazi (asilimia 70) kutoka maeneo ya Kaskazini Mashariki waliohojiwa katika utafiti huo walisema kuwa wanafuatilia watoto wao wanapocheza na wenzao kuhakikisha kuwa hawatangamani na kujiweka katika hatari ya kuambukizana virusi vya corona.