• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Waziri ajiuzulu baada ya njama yake ya kufurusha wahamiaji Uingereza kuanikwa

Waziri ajiuzulu baada ya njama yake ya kufurusha wahamiaji Uingereza kuanikwa

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Amber Rudd alijiuzulu Jumapili jioni akikiri kuwapotosha wabunge kuhusu makataa ya kuwafurusha wahamiaji haramu nchini humo.

Hii ni kutokana na sakata ya Windrush ambayo ilimshinikiza Bi Rudd na kukosolewa vikali kuhusu iwapo alijua kuhusu mipango ya wizara yake ya kuwafurusha wahamiaji.

Gazeti la Guradian lilichapisha barua ambayo Bi Rudd alimwandikia Waziri Mkuu Theresa May kuhusu lengo lake “lenye maono magumu lakini yanayoweza kutekelezwa” la kufurusha asimilia 10 zaidi ya wahamiaji haramu katika “miaka michache ijayo”.

Bi Rudd, ambaye alikuwa ameratibiwa kuhutubia bunge la Commons, alimpigia Bi May simu na kumwarifu kuhusu uamuzi wake wa kujiengua madarakani huku shinikizo kutoka kwa upinzani zikichacha.

Katibu wa wizara hiyo Diane Abbott alisema “mhusika mkuu wa njama hii” – ambaye ni waziri mkuu – anafaa kufika mbele ya bunge kuelezea iwapo alijiua kuwa Bi Rudd aliipotosha bunge.

Kabla ya kujiuzulu kwake, chama chake cha Tory kilikuwa kinamtetea kuhusu sakata hiyo.

Kando na kukosa kumakinika, jambo lingine lililompa presha Bi Rudd lilikuwa kwamba alikosa uhusiano wa kirafiki na waziri waliyemtangulia, hasa kuhusu suala zima la uhamiaji.

Mzozo wa Windrush ulianza wakati iliibuka kuwa baadhi ya wahamiaji waliotoka mataifa yaliyotawaliwa na Uingereza, waliohamia humo kati ya 1940 na 1970, pamoja na familia zao, walikuwa wametangazwa kuwa wahamiaji haramu.

Akisifu kujiuzulu kwake, mbunge wa Labour David Lammy alisema: “Amber Rudd amejiuzulu kwa kuwa hakuelewa kilichokuwa kikifanyika katika wizara yake, na alikuwa amepoteza imani ya watu aliowasimamia.

“Suala muhimu ni sera ya mazingira ambayo ilizua utata mwanzoni. Sera hiyo sasa inafaa kubadilishwa, na Wizara ya Mambo ya Ndani inafaa kuwa mbioni kuwapa uraia watu wa kizazi cha Windrush.”

Wabunge wa Conservative nao wamekuwa wakimmiminia sifa mwenzao.

Kiongozi wa Bunge Andrea Leadsom alisema Bi Rudd ni “mkweli na aliyestaarabika” huku katibu wa jamii Sajid Javid akisema Bi Rudd alikuwa na “kipaji cha juu” na “bila shaka atarudi kwenye Baraza la Mawaziri hivi karibuni”.

Waziri wa Mambo ya Kigeni Bw Boris Johnson alisema waziri huyo “alifanya kazi nzuri wakati wa shambulio la kigaidi mwaka jana na anawajali sana watu anaohudumia”.

You can share this post!

Kipruto aongoza kwa kasi mbio za kilomita 10 mwaka huu

Pompeo ajikuna kichwa kupatanisha Israeli na Palestina

adminleo