Habari Mseto

Sababu za mbunge wa Mvita kupinga agizo la usafirishaji kontena kutumia SGR

June 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na FARHIYA HUSSEIN

MBUNGE wa Mvita, Kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir amepinga agizo la serikali la kutumia reli mpya na ya kisasa SGR kutumiwa katika usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Mombasa hadi Naivasha.

Akiongea na Taifa Leo kwa njia ya simu, mbunge huyo alisema kwamba uamuzi wa Waziri wa Usafiri na Uchukuzi, Bw James Macharia unalenga kuathiri uchumi wa Mombasa kwa njia hasi.

“Hawawezi kusema sababu kuu ya kuamua usafirishaji wa mizigo kutoka Mombasa kuelekea Naivasha kupitia SGR ni njia ya kupunguza kuenea kwa Covid-19 ilhali bidhaa hizo zitachukuliwa na madereva wa malori ambao tunapambana mchana na usiku kuhakikisha wanakuwa salama kiafya,” alisema.

Akaongeza: “Hii ni mara ya tatu hili kutokea. Ni muhimu suluhisho la kudumu au sheria sahihi kupatikana ili kuondoa utata.

Alilalamika zaidi kuwa haitaathiri Mombasa tu lakini pia miji mingine kama Mtito Andei, Voi, na miji mingine mikubwa.

“Sio suala la usafirishaji tu. Kuna mengi sana yanayohusika kama vile vifaa (logistics) na maghala (warehousing). Wakati serikali inasema hivyo, basi kampuni hizo ambazo zinapendelea shehena zao zote zihifadhiwe katika sehemu moja huko Mombasa zitaathirika pakubwa,” alisema Bw Shariff.

Kulingana na mbunge huyo, serikali haipaswi kutumia Dongo Kundu kama njia ya kutatua suala la SGR.

“Hatuwezi kukaa kimya mpaka wakati huo. Dongo Kundu linatarajiwa kuanza kazi kwa muda wa miaka mitano kutoka leo. Tukakaa vipi kimya wakati uchumi wa mkoa wa pwani unazidi kudhoofika, “alisisitiza Bwana Shariff.

Pia, Bw Shariff alimkosoa vikali waziri kwa kulaumu Mombasa kama kitovu cha Covid-19 na kwamba “inapaswa kuepukwa na wafanyabiashara.”

Serikali imekuwa ikikabiliwa na upinzani kutoka kwa viongozi wa Pwani kwa miaka miwili sasa kuhusu suala la kutumia SGR kusafirisha mizigo kutoka Mombasa hadi Naivasha