Habari MsetoSiasa

Ishara zote zaonyesha Waiguru ataepuka balaa

June 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CHARLES WASONGA na VALENTINE OBARA

WANDANI wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, Jumanne walionyesha ishara za nia ya kumwokoa Gavana wa Kirinyaga, Bi Anne Waiguru dhidi ya kung’olewa mamlakani.

Katika ushindi wao wa kwanza dhidi ya mahasimu wa Bi Waiguru, walifanikiwa kumwepushia kibarua cha kujitetea mbele ya kikao kizima cha seneti na badala yake wakapiga kura kwa wingi ili kamati maalumu iundwe kuamua suala hilo.

Majibizano makali yalishuhudiwa jana kati ya maseneta wanaounga mkono handisheki na wale wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto ambao walikuwa wanapigia debe hoja ya kumng’oa gavana huyo iamuliwe na seneti nzima.

Seneta wa Siaya, Bw James Orengo ambaye pia ndiye Kiongozi wa Wachache alitoa ishara kwamba chama hicho kitamtetea Bi Waiguru hadi mwisho.

“Kuna watu hawatafuti haki. Kichwa cha Waiguru hakitafutwi na bunge la Kaunti ya Kirinyaga bali ni watu wengine wanaomtafuta. Nina ushahidi kuhusu hilo,” akadai.

Kwa upande wake, Seneta wa Pokot Magharibi aliye Kiongozi wa Wengi, Samuel Poghisio, alitetea uundaji wa kamati maalumu akisema kamati hiyo itawakilisha msimamo wa Seneti nzima.

Lakini wafuasi wa Tangatanga waliotaka hoja ya Bi Waiguru isikizwe na kikao kizima cha Seneti walilalamika.

“Wakazi wa Kirinyaga wamekuwa wakishuku kuwa uamuzi tayari umfanywa kuunda kamati ya kumhoji Waiguru na matamshi ya Orengo yamethibitisha hilo. Kama kamati ya kumtakasa Waiguru iliundwa tuambiwe mapema,” akasema Seneta wa Elgeyo Marakwet, Bw Kipchumba Murkomen.

Katika uamuzi uliotolewa, maseneta 45 walipiga kura kukubali kamati iundwe nao 14 wakapinga huku mmoja akasusia kura.

Hii ni licha ya wakazi wa Kirinyaga kuandamana mjini Kerugoya wakitaka Seneti iwatendee haki bila kushawishiwa na mamlaka za nje.

Wanachama wa kamati iliyoundwa watahitajika kushughulikia hoja hiyo ndani ya siku 10.

Wanajumuisha Paul Mwangi Githiomi (Nyandarua), Michael Mbito (Trans Nzoia), Anuar Loitiptip (Lamu), Philip Mpaayei (Kajiado), Cleophas Malala (Kakamega), Stewart Madzayo (Kilifi) na Moses Kajwang (Homa Bay). Wengine ni Maseneta Maalum Beatrice Kwamboka, Judith Pareno, Abishiro Halake, na Beth Mugo.

Bi Waiguru ataponea chupuchupu ikiwa angalau wanachama sita watatupilia mbali tuhuma dhidi yake baada ya kupokea ushahidi na gavana kujitetea.

Kamati hiyo itafanya vikao vya hadhara ambapo wawakilishi wa pande zote mbili wataalikwa. Bunge la Kirinyaga linaweza kuwakilishwa na wakili wao, spika au madiwani walioteuliwa na wenzao.

Watahitaji kuwasilisha ushahidi walio nao dhidi ya Gavana Waiguru kwa kamati hiyo kupitia afisi ya karani wa seneti Bw Jeremiah Nyengenye saa 24 kabla ya kufika mbele ya kamati.

Gavana Waiguru atahitajika kufika binafsi mbele ya kamati hiyo kujitetea, atume wakili wake, au afike akiandamana na wakili wake.

Ikiwa Kamati hiyo itabaini kuwa mashtaka dhidi ya Gavana Waiguru yana mashiko, itaandaa ripoti na kuiwasilisha kwa kamati ya maseneti wote ili ijadiliwe.