• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Wazazi washauriwa wasiwe wakifarakana mbele ya watoto wao

Wazazi washauriwa wasiwe wakifarakana mbele ya watoto wao

Na MISHI GONGO

MAAFISA katika idara za watoto mjini Mombasa wamewataka wazazi kutogombana mbele ya watoto wao, wakisema hali hii huwaathiri watoto kisaikolojia.

Wakizungumza katika Maadhimisho ya Mtoto wa Kiafrika walisema zaidi ya watoto 52 wameokolewa kutoka mitaani baada ya kutoroka majumbani mwao kufuatia mizozo kati au baina ya wazazi.

Afisa wa watoto mjini Mombasa Bw Philip Nzege alisema kufuatia mafarakano ya wazazi, baadhi ya watoto huamua kutoroka na kuanza maisha barabarani.

“Wanapokuwa mitaani, wanajiweka katika hatari mbalimbali zikiwemo kunajisiwa, kushawishiwa kushiriki katika utumiaji wa mihadarati na hata kupewa mimba za mapema,” akasema.

Aliwaomba wazazi kuhakikisha wanatatua mizozo yao mbali na watoto.

Bi Selina Maitha afisa wa polisi aliyeongea kwa niaba ya kamishna wa Mombasa Bw Gilbert Kitiyo, alisema tangu kuzuka kwa janga la Covid-19 watoto mjini Mombasa wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali.

Aidha aliwaonya wazazi wanaowatumia watoto wao kama vitega uchumi.

Alisema baadhi ya wazazi wanawatumia watoto kuokota chupa barabarani kwa akili ya kuuza bila kuzingatia hali yao ya afya.

“Katika doria zetu tunakutana na watoto wanaokota chupa na vyuma barabarani bila maski ambapo tunapowashika na kuwadadisi watoto hao husema kuwa wametumwa na wazazi wao,” akasema.

Hata hivyo, alisema wameungana na wazee wa mitaa kuhakikisha kuwa watoto hawadhulumiki mitaani nyakati hizi ambapo shule zimefungwa.

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kiafrika husherehekewa kila mwaka baina ya Juni 15 na Juni 16 kuwakumbuka watoto walioleta mageuzi mwaka 1976 Soweto, Afrika Kusini.

You can share this post!

VINYWAJI: Jinsi ya kuandaa smoothie ya parachichi

Vilio watoto 4,000 wakipachikwa mimba Machakos

adminleo