Mama ashangaza kuuza mwanawe kwa Sh28,000
Na James Murimi
MWANAMKE jana alishtakiwa katika Mahakama ya Nanyuko kwa madai ya kuuza mtoto wake wa kike, 5, kwa Sh28,580. Bi Esther Ekale, 26, alishtakiwa pamoja na wanawake wawili ambao ilidaiwa walishiriki katika biashara hiyo haramu.
Mahakama iliambiwa kuwa mnamo Juni 13, mjini Naromoru, Kaunti ya Nyeri, Bi Ekale alipokea pesa hizo kutoka kwa Bi Jane Watare aliyemtaka mtoto huyo.
Kwa upande mwingine, Bi Jane Wanjiru alishtakiwa kwa madai ya kupanga jinsi malipo hayo yangefanywa kwa Bi Ekale.
Watatu hao walikanusha mashtaka mbele ya Hakimu Mwandamizi, Bi Njeri Thuku.
Kiongozi wa Mashtaka, Bi Virginia
Kariuki, aliambia mahakama kuna watu wanne ambao wamejitolea kuwa mashahidi katika kesi hiyo.
Bi Thuku aliagiza idara ya watoto kuandika ripoti kumhusu mtoto huyo, na nyingine iandikwe kuhusu washtakiwa hao watatu.
Hakimu pia aliagiza Bi Wanjiru apelekwe hospitalini kwani alilalamika kwamba anaugua.
Mahakama iliagiza washtakiwa wazuiliwe katika Kituo cha Polisi cha Naromoru hadi Julai 8, 2020 wakati kesi itakapotajwa.