• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
Naibu Kamishna mpenda hongo abambwa kwa utapeli wa mashamba

Naibu Kamishna mpenda hongo abambwa kwa utapeli wa mashamba

NA MWANGI MUIRURI

NAIBU Kamishna katika Kaunti ya Murang’a amekamatwa na maafisa wa kupambana na ufisadi kwa madai ya utapeli wa mashamba.

Bw Alex Mukindia akiwa Msaidizi wa Kamishna katika tarafa ya Maragua alijipata taabani Jumanne baada ya mkubwa wake Mohammed Barre ambaye ndiye Kamishna kuagiza akamatwe muda mfupi baada ya mjane kuwasilisha malalamishi afisini mwake kuwa msaidizi huyo ni mfisadi.

Barre alifichua kuwa afisa huyo alituhumiwa kujaribu kushirikisha njama ya utapeli wa shamba la mjane huyo ambapo alikataa kutoa idhini ya umiliki kabla hajapokezwa Sh40,000.

Eneo la Maragua linafahamika vyema kwa visa tele vya utapeli wa mashamba ambao hushirikishwa na mitamndao ya ukora ambayo huyjumuisha wanasiasa, maafisa wa kiserikali na wafanyabiashara pamoja na madalali.

Alinaswa afisini mwake katika Mji Wa Maragua na kuwasilishwa hadi makao makuu ya maafisa hao Mjini Murang’a ambapo aliandikisha taarifa na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh50, 000 huku akingojea maelekezi zaidi baada ya uchunguzi kukamilika.

Mukindia ambaye amekuwa akitajwa katika visa vingine kadhaa vya utapeli wa mashamba, alijipata taabani baada ya baadhi ya waathiriwa kukataa kutoa hongo ili awasaidie na wakajitokeza kwa afisi ya Kamishna kulalamika.

Hadi kukamatwa kwake, alikuwa amepokezwa barua ya uhamisho hadi Kaunti ndogo ya Kikuyu ndani ya Kiambu na ambapo alikuwa apokeze majukumu yake rasmi kwav mrithi wa afisi hiyo.

Malalamishi yaliyowasilishwa ni kuhusu Bi Hannah Kabui aliyekuwa ameuza ploti ya upana wa futi 80 kwa 120 kwa Bi Winnie Wanjiku. Upana wote wa shamba la Bi Kabui ulikuwa ni ekari 0.6.

Katika stakabadhi za kutoa ploti hiyo, kuna ukora ulifanyika ambapo Bi Kabui (muuzaji)alibakia kuwa ndiye mumiliki wa ploti hiyo huku Bi Wanjiku (mnunuzi) akisemwa kuwa ndiye alikuwa mumiliki wa shamba kubwa lililosalia baada ya ploti hiyo kutolewa.

Lakini Bi Wanjiku alikataa kushirikishwa katika ukora huo wa kumtapeli Bi Kabui shamba lake.

“Mimi sikutaka nikule vya haramu kutoka kwa mjane huyu mkongwe na nikazindua harakati za kumsaidia ili stakabadhi zetu zilainishwe,” Bi Wanjiku akaambia Taifa Leo.

Ni katika harakati za kusaka njia ya kutatua hitilafu hiyo ambapo Bi Wanjiku alipata mteja wa kununua ploti hiyo na wakaafikiana kwamba katika stakabadhi mpya za umiliki, hitilafu hiyo irekebishwe.

“Niliuza ploti hiyo kwa kikundi cha kijamii cha Maragua Aviation na tukakubaliana kwamba stakabadhi mpya zionyeshe Bi Kabui kama mumiliki wa shamba lake halali. Baada ya kufuata mkondo wote wa kisheria wa kubadili umiliki, Bw Mukindia alikatalia idhini hiyo ya kuhalalisha kubadilishwa kwa majina ya umiliki,” akasema Bi Kabui.

Maafisa wa Maragua Aviation waliambia Taifa Leo kuwa Bw Mukindia alikataa katakata kutoa idhini hiyo akidai kuwa apokezwe Sh40, 000 kama hongo ambayo ilikuwa ichangwe na Bi Kabui, Bi Wanjiku na Maragua Aviation.

Ndipo walikataa na wakawasilisha malalamishi kwa afisi ya Kamishna wa Kaunti na ambaye alielekeza maafisa wa kupambana na ufisadi wamwendee Bw Mukindia.

You can share this post!

UhuRaila wakejeliwa kwa ‘kutakasa ufisadi’

Yafichuka Ikulu inalazimisha Mlima Kenya kuunga mkono BBI

adminleo