• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
Hofu ya ‘Jicho Pevu’ akitaka kung’oa waziri mamlakani

Hofu ya ‘Jicho Pevu’ akitaka kung’oa waziri mamlakani

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Nyali Mohammed Ali sasa ameingiwa na hofu baada ya kuwasilisha hoja ya kutaka kumng’oa afisini Waziri wa Uchukuzi James Macharia.

Bila kutaja majina ya wahusika, Bw Ali alidai ana habari kwamba hoja yake imewakera watu fulani ambao anashuku wanaweza kumdhuru.

“Hii ndio maana sasa namwomba Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai kuimarisha usalama wangu hapa Nairobi na kule Mombasa ili watu kama hao wasinizuie kutekeleza wajibu wangu, kama mbunge, wa kuwatetea wanyonge,” akasema akiongeza kuwa atapiga ripoti rasmi kwa polisi kuhusu suala hilo.

Awali, zaidi ya wabunge 30 kutoka mirengo ya Jubilee na Nasa walipuuzilia mbali hoja hiyo wakidai Bw Ali anaendeleza hila na chuki dhidi ya Waziri Macharia kupitia hoja hiyo.

“Hii hoja haina mashiko yoyote kwani haijaandamanishwa na masuala yenye mashiko kulingana na Katiba na sheria husika za nchi. Tunamwomba Spika asiidhinishe hoja hiyo kwa sababu nia ya mwenzetu Bw Ali ni kumchafulia jina Waziri Macharia ambaye amekuwa akifanya kazi nzuri,” akasema Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.

Naye Mbunge wa Igembe Kusini Paul Mwirigi alidai kuwa Bw Ali alimhadaa kutia saini hiyo kwa kumwambia kuwa ilikuwa fomu ya kuomba mkopo kutoka kwa shirika la akiba na mikopo la Bunge.

“Nimemwandikia Spika wa Justin Muturi kuondoa sahihi baada ya kugundua kuwa mwenzangu alidanganya,” akasema Bw Mwiriga.

Hata hivyo, sheria za bunge hazimruhusu mbunge kuondoa sahihi yake katika hoja kama hiyo.

Mnamo Jumatano Bw Ali aliwasilisha hoja yake kwa afisi ya karani wa bunge la kitaifa Michael Sialai pamoja na sahihi 90 alizokusanya kutoka kwa wabunge wanaounga mkono azma yake.

Miongoni mwa tuhuma anazomwelekezea Bw Macharia ni amri ya wizara yake kwamba sharti mizigo isafirishwe kutoka bandari ya Mombasa kupitia reli ya kisasa, SGR, hadi eneo kihifadhia makasha la Naivasha.

Bw Ali anasema Waziri alitoa amri hiyo bila ya kuhusisha maoni ya viongozi wa pwani na umma kinyume cha kipengee cha 10 cha Katiba.

Aidha, anadai Bw Macharia amepotoka kimaadili kwa misingi ya kukwama kwa miradi ya thamani ya Sh100 bilioni inayotekeleza chini ya wizara yake. Bw Ali pia amemhusisha waziri huyo na sakata ya Sh5 bilioni iliyotokea katika wizara ya afya mnamo 2017 chini ya usimamizi wake kama waziri.

You can share this post!

Misongamano mipakani kupandisha bei ya unga

Msanii Omondi Long Lilo kuzikwa leo

adminleo