• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 2:13 PM
Hatuko pamoja!

Hatuko pamoja!

Na MWANGI MUIRURI

WANDANI wa Naibu Rais William Ruto, wamefichua kuwa wanajiandaa kuendeleza mikakati ya kumpigia debe licha ya kuadhibiwa na viongozi wanaoegemea upande wa Rais Uhuru Kenyatta.

Huku wafuasi hao wa mrengo wa Tangatanga wakiendelea kuadhibiwa kutokana na madai ya kuhujumu ajenda za Rais na kufanya kampeni za mapema, wameonyesha dalili za kuunda chama kipya ambacho huenda kikatumiwa na Dkt Ruto kuwania urais ifikapo mwaka wa 2022.

Mnamo Alhamisi, Dkt Ruto alikutana na washirika wake 20 katika afisi mpya ambayo wameibandika jina ‘Jubilee Asili Centre’ katika mtaa wa Kilimani, Nairobi. Washirika hao wanajumuisha wabunge na maseneta ambao walipokonywa nyadhifa zao za kuongoza chama bungeni.

Wameamua kujitenga na shughuli za Chama cha Jubilee zinazoendelezwa katika makao makuu ya chama hicho katika eneo la Pangani ijapokuwa hawatarajiwi kukihama kwa sasa, kwani watakuwa wanahatarisha kupoteza nyadhifa zao za uongozi.

Naibu Mwenyekiti wa Jubilee, Bw Caleb Kositany ambaye ni mwandani mkubwa wa Dkt Ruto, alisema kuwa wafuasi wake wote wanafaa wawe watulivu wakisubiri matukio ambayo yataanza kutekelezwa kutoka kwa mikutano ya Jubilee Asili.

“Tuko katika safari hii ya Dkt Ruto hadi mwisho wake na hatujalishwi na hila na njama za wenzetu ndani ya Jubilee ila tu waelewe tutapambania nafasi yetu ndani ya Jubilee na pia uwaniaji wa urais katika mwaka wa 2022,” akasema.

Alisema maazimio ya Jubilee kama ilivyokuwa tangu 2013 hadi 2017yangalipo lakini kwa sasa yatafufuliwa na kuimarishwa ndani ya Jubilee Asili.

Baadhi ya maamuzi ambayo alisema yatatolewa kutoka afisi hizo mpya ni kuhusu msimamo wao halisi kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI), uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Jubilee na msimamo kuhusu hoja za bunge.

Naibu mwenyekiti wa Jubilee, Bw David Murathe jana alionya kuwa, kwa kuanzisha vuguvugu la Jubilee Asili, wafuasi wa Tangatanga wanajiweka hatarini kutimuliwa chamani.

“Hatua ya wandani wa Ruto kuunda mrengo pinzani ni ishara tosha kwamba wamejiondoa serikalini. Sasa wanafaa kuchukuliwa kama waasi na kutimuliwa ili Rais aunde serikali mpya iliyo na washirika wapya,” akasema.

Ingawa Bw Murathe alishikilia kuwa Dkt Ruto hatatimuliwa kwa lazima kutoka wadhifa wake wala kutoka Chama cha Jubilee kwa sasa, alisema angefaa kujiondoa kwa hiari ili “akajenge nyumba yake mpya ya Jubilee Asili”.

Mbunge wa Kikuyu, Bw Kimani Ichung’wa, alimpuuzilia mbali Bw Murathe na kusema yeye ni mmoja wa watu ambao wamesambaratisha maazimio yaliyokuwa ya Jubilee awali.

“Ni wazi kuwa Chama cha Jubilee kimetekwa nyara na watu wanaojifanya wana hatimiliki ya makao makuu. Jubilee inadhibitiwa na watu wanaobagua wengine ndani ya chama,” akasema.

Alisema hali hiyo ndiyo imewafanya wafuasi wa Dkt Ruto wanaoamini wao ndio waasisi halali na asili wa chama cha Jubilee, kupendekeza vuguvugu jipya la Jubilee Asili ambalo kwalo watatoa mwelekeo kwa wafuasi wao katika siku zijazo.

Alifafanua kuwa kwa sasa Jubilee Asili si chama kwa kuwa kisheria hawawezi kuwa ndani ya vyama vingine kabla ya awamu yao ya uongozi kukamilika wakati bunge litakapovunjwa ili uchaguzi mwingine ufanywe. “Tumeunda tu mahali petu pa faragha ya kukutana kama wafuasi wa Dkt Ruto,” akasema.

Mwandani mwingine wa Dkt Ruto aliyeomba asitajwe jina, alisema Jubilee Asili “ni mwanzo tu wa ngoma, lele yaja”.

“Umaarufu wa Dkt Ruto umekuwa ukipanda kila uchao na kwa kiwango cha juu kiasi kwamba wanaompinga wamekuwa wakizindua njama na hila za kuhujumu uwezekano wa nyota yake ya 2022 kung’aa zaidi,” akasema.

Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen alisema kuwa kwa sasa “tumeamua kukomesha vurugu na ubishi wa afisi kwa kujipa hifadhi yetu ya kukutana bila masharti”.

“Kutokana na kuwa tumeonyeshwa uchokozi wa hali ya juu na ukatili si haba na wenzetu ndani ya Jubilee, tumeona ni vyema tuwape majenerali wetu mahala patulivu pa kupangia mikakati yetu ya baadaye,” akasema mbunge huyo kutoka eneo la Kati.

Mbunge wa Kimilili, Bw Didimus Baraza aliambia Taifa Leo kwamba: “Ndoa ikivunjika ni lazima anayeteswa ajipe hifadhi mbadala ili kuepukana na mvurutano usio na manufaa.”

You can share this post!

Nondies kuhamia uwanja mpya

Wabunge wakataa ushuru kwa pensheni

adminleo