Habari MsetoSiasa

Kibwana na Muthama wazika tofauti zao

June 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

BENSON MATHEKA na PIUS MAUNDU

GAVANA wa Makueni Kivutha Kibwana na aliyekuwa seneta wa Machakos Johnson Muthama wamezika tofauti zao na kuamua kushirikiana kisiasa.

Viongozi hao waliokuwa mahasimu wa kisiasa walikutana wiki hii na kusema kuwa lengo lao ni kuunganisha jamii ya Wakamba na kuhakikisha kaunti tatu za eneo lao haziachwi nyuma kimaendeleo.

“Nilikutana na Mheshimiwa Muthama na tukajadili uongozi wa eneo letu. Nilitaka kujua alichomaanisha aliposema kwamba uongozi wa eneo letu umebadilika. Tulijadili muungano wa kiuchumi wa kaunti za eneo la Kusini Mashariki la Kenya na masuala mengine ya maendeleo,” Bw Kibwana alisema kwenye mahojiano na Taifa Jumapili.

Wawili hao wamekuwa wakikutana kwa siri hasa baada ya Bw Muthama kumsifu Bw Kibwana na kumtaja kama kiongozi shupavu anayeweza kuongoza jamii ya Wakamba. Duru zinasema kuwa wawili hao walijadili juhudi za kumtimua Gavana wa Kitui Charity Ngilu zinazoendelezwa na madiwani wa chama cha Wiper.

Bw Kibwana amekuwa akimlaumu kiongozi wa chama hicho Kalonzo Musyoka kwa kuchochea mizozo kati ya madiwani na magavana wa kaunti za Makueni, Machakos na Kitui. Alitofatutiana na makamu huyo wa rais wa zamani alipotangaza ushirikiano wake na Rais Uhuru Kenyatta.

Mwishoni mwa mwaka jana, Muthama pia alitofautiana na Bw Musyoka kwa kukubali kuwa mtu wa mkono wa Rais Kenyatta bila kujali maslahi ya jamii.

Mkutano wa Jumatano, ulijiri wakati Musyoka aliongoza chama cha Wiper kutia sahihi mkataba wa ushirikiano na chama tawala cha Jubilee na madiwani wa bunge la kaunti ya Kitui wakipanga kumtimua Gavana Ngilu.

Kulingana na aliyekuwa Naibu Gavana wa Machakos Benard Kiala ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Muthama, viongozi hao wamekuwa waKijadili masuala ya uongozi na maendeleo eneo la Ukambani.

“Ninaweza kuthibitisha kuwa mkutano huo ulihusu uongozi na muungano wa kiuchumi wa kaunti za Kusini Mashariki mwa Kenya,” Bw Kiala alisema.

Muthama ameashiria kuwa huenda akamuunga Bw Kibwana kuwa msemaji wa jamii ya Wakamba akisema Bw Musyoka ametelekeza wajibu huo kwa kukosa kushauriana na viongozi wengine kabla ya kufanya maamuzi muhimu.

“Profesa Kibwana anatosha kuwa waziri mkuu au Naibu wa waziri mkuu katiba ikibadilishwa. Amethibitisha kuwa ni kiongozi jasiri anayeweza kutegemewa,”alisema Bw Muthama.

Amekuwa akimtaja Bw Musyoka kama kiongozi mbinafsi tangu alipokanusha kuwa na mpango wa kuungana na Naibu Rais William Ruto na kukariri ushirikiano wake na Rais Kenyatta.

Baada ya Muthama kutofautiana na Musyoka, Profesa Kibwana alimtaja Kama shujaa wa jamii ya Wakamba. Wadadisi wanasema ukuruba wa kisiasa kati ya Muthama na Ngilu umechochewa na hisia la kuwepo kwa pengo katika uongozi eneo la Ukambani baada ya Musyoka kukumbatia chama tawala.