Mudavadi na Weta wapigania ubabe Magharibi
BENSON AMADALA na DERICK LUVEGA
MIPANGO ya kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula kukabili kampeni za Waziri wa Ugatuzi, Eugene Wamalwa na Gavana Wycliffe Oparanya wa Kakamega katika eneo la magharibi, zimeibua mvutano mpya.
Washirika wa Naibu Rais William Ruto sasa wametangaza kuwaunga mkono Bw Mudavadi na Wetangula katika makabiliano ya pande hizo mbili kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.
Wabunge wa ANC, Ford Kenya na Jubilee wamewashtumu Bw Wamalwa na Oparanya kwa kutumiwa na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) kuwahujumu Bw Mudavadi na Wetangula, ambao wanachukuliwa kuwa wanasiasa waliobobea eneo hilo.
Bw Wamalwa na Oparanya katika muda wa majuma mawili yaliyopita, wamezuru kaunti za Bungoma, Busia na Vihiga na kufanya mikutano na wazee wa eneo hilo kutafuta mwelekeo wa kisiasa wakijaribu kuunga ajenda za maendeleo za Rais Uhuru Kenyatta.
Walisema lengo lao ni kutambua mahitaji ya kimaendeleo na kushinikiza ugawaji wa rasilmali kwa miradi ya kuimarisha maisha.
Mnamo Jumamosi, mkutano uliopangwa kuongozwa na viongozi hao wa ANC na Ford Kenya eneo la Malava, ulikatizwa na polisi kwa hofu ya kukiuka masharti ya kuzuia maambukizi ya corona.
Lakini wawili hao wameshtumu polisi kwa kutekeleza sheria kwa mapendeleo.
“Wakati waziri Wamalwa na Gavana Oparanya walikuwa wakikutana na wazee wakihutubia mikutano kwa dai la kusambaza chakula cha msaada kwa familia zilizoathiriwa na mafuriko na Covid-19, hawakuwa wanakiuka kanuni?” aliuliza Bw Mudavadi.