Mwalimu mstaafu apoteza kesi aliyopigania kwa miaka 19
Na RICHARD MUNGUTI
MAHAKAMA ya rufaa imetupilia mbali kesi iliyosikizwa na majaji wengi zaidi ya mwalimu mstaaafu ambaye amepigania nyongeza ya pensheni yake kwa muda wa miaka 19.
Wakitupilia mbali kesi hiyo Majaji Philip Waki, Fatuma Sichale na Sankale ole Kantai walisema kesi ya Bw Jimnah Mwangi Gichanga iliwasilishwa mara sita kortini na “kila wakati imetupwa.”
Bw Gichanga amekuwa akiomba korti iamuru Serikali alipwe pensheni ya kiwango cha juu kufuatia kuimarishwa kwa malipo ya pensheni katika mwongozo mpya.
Majaji hao walisema Bw Gichanga mwenye bidii ya mchwa amepambana na Serikali na tume ya kuajiri walimu (TSC) pasi kusaidiwa na wakili kwa miaka hiyo yote.
“Mlalamishi alishindwa kuwasilisha ushahidi kuthibitisha anastahili kulipwa pensheni kwa kiwango cha ajira cha R,” walisema majaji hao.
Majaji Waki, Sichale na ole Kantai walisema licha ya Bw Gichanga kuwasilisha kesi mara nyingi hivyo kile alikataa kuelewa ni kuwa hakuwa amehitumu kulipwa mshahara katika kiwango cha ajira cha R badala ya K.
Bw Gichanga aliyestaafu mwaka wa 1999 baada ya kufanyakazi ya ualimu kwa miaka 37 akiwa kwa kiwango cha ajira cha K. Amekuwa akilipwa pensheni kwa kiwango cha Ajira cha K.
Amekuwa akipigania alipwe pensheni ya kiwango cha R akisema alihitimu kwa shahada ya Digirii.
Kesi hiyo ilisikizwa katika Mahakama kuu na pia katika Mahakama ya kuamua mizozo ya wafanyakazi (ELRC) na Majaji Ruth Sitati , Murugi Mugo (jaji mstaafu), Andrew Hayanga (jaji mstaafu) , Monicah Mbaru. Majaji ambao walitupilia mbali kesi hiyo.
Katika mahakama ya rufaa kesi hii ilisikizwa na Majaji Waki, Sichale, ole Kantai, Majaji wastaafu Riaga Omolo na Onyango Otieno. Wengine walioisikiza ni Majaji Hannah Okwengu, William Ouko, Kathurima M’Inoti na Jaji wa Mahakama ya Juu Mohammed Ibrahim.
Mahakama ilisema kesi hiyo iliamuliwa kabisa na Jaji Sitati 2009 alipoitupilia mbali akisema hakuna ushahidi wowote ambao mlalamishi aliwasilisha kuiwezesha kuamuru Serikali imwongezee pensheni yake.
Mahakama ilisema mlalamishi amechukua muda mrefu kuelewa maamuzi yaliyotolewa na korti.
Walisema pia mlalamishi alichanganya kesi nyingi pamoja na ushahidi.