Mifugo Samburu wachanjwa
Na GEOFFREY ONDIEKI
Serikali imeanzisha kampeni ya kutoa chanjo ya ugonjwa wa miguu na mdomo katika kaunti ya Samburu.
Kampeni hiyo inalenga kuchanja mifugo takriban 900,000 kwenye kaunti hiyo ambayo wakazi wengi hutegemea ufugaji ili kujikimu kimaisha.
Idara ya mifugo pia inatarajia kutoa chanjo kwenye kaunti 14 ambazo zimeripoti visa kadha vya magonjwa ya mifugo.
Kaunti hizo ni pamoja na Samburu, Isiolo, Laikipia, Kajiado, West Pokot na nyinginezo.
Awamu ya kwanza ya zoezi hilo, ambalo lilizinduliwa wiki iliyopita na waziri wa Kilimo Peter Munya, litachukua siku 14 kukamilika.
Katibu mwandamizi katika Wizara ya Kilimo Linah Jebii Kilimo ambaye alizindua mpango huo katika kaunti ya Samburu, alisema kuwa asilimia 80 ya wanyama wote katika kaunti hiyo watachanjwa kwa minajili ya kuzuia usambazaji wa magonjwa.
Afisa huyo alifichua kwamba taifa la Kenya linapitia hali ngumu kuyakabili magonjwa ya mifugo, ambayo pia yamelemaza juhudi za biashara ya mifugo kutoka kaunti jirani.
“Tumeanzisha kampeni kwenye kaunti 14 ikiwemo Samburu na itatusaidia kukabiliana na ugonjwa wa miguu na mdomo na magonjwa mengine na kuinua usalama wa chakula ambao ni muhimu katika taifa letu,” alisema Bi Jebii.
Alikiri kuwa asilimia 90 ya wakazi katika kaunti ya Samburu ni wafugaji na hutegemea biashara ya mifugo kujipatia riziki ya kila siku.
Alihimiza serikali ya kaunti ianzishe juhudi za kukomesha magonjwa ya mifugo ambayo yanaangamiza mifugo kila kuchao.